"Huwa natamani mama angekuwepo" Moji Short Baba afunguka uchungu wa kumpoteza mamake

Muhtasari

•Moji alisema huwa anatamani sana mzazi huyo wake bado angekuwepo ajionee maendeleo ya maisha yake.

•Moji alisema mama yake aliaga dunia wakati ambao alikusudia  kumlipa kwa malezi bora aliyompa. 

Image: INSTAGRAM// MOJI SHORT BABA

Mwimbaji wa nyimbo za injili James Muhia almaarufu kama Moji Short Baba amekiri kwamba hajawahi kupata nafuu tangu ampoteze mama yake mwaka wa 2014.

Akiwa kwenye mahojiano na SPM Buzz, Moji alisema ilikuwa ngumu sana kwake kukabiliana na kifo cha mzazi huyo wake.

"Wakati alifariki ndio nilikuwa najaribu kutoboa maishani.Ndugu zangu walikuwa wadogo sana. Ilikuwa ngumu. Bado ni ngumu. Kupoteza mama sio jambo ambalo unaweza kusahau. Ni mojawapo ya mambo magumu zaidi ambayo nimewahi kupitia," Moji alisema.

Mwanamuziki huyo ambaye alifunga ndoa mwaka jana alifichua kwamba huwa anamkumbuka sana mamake. Alisema huwa anatamani sana mzazi huyo wake bado angekuwepo ajionee maendeleo ya maisha yake.

"Nikifanikiwa huwa natamani mama angekuwepo. Nikipitia wakati mgumu huwa natamani mama angekuwepo kuniongelesha. Hata hivyo nashukuru Mungu kwa kuwa amekuwepo. Ameleta  watu wa kunisaidia kujishikilia," Alisema.

Moji alisema mama yake aliaga dunia wakati ambao alikusudia  kumlipa kwa malezi bora aliyompa. Alieleza kwamba nyanyake alijaza pengo ambalo mama yake aliaacha.