'Nilikaa nyumbani miezi 6,' DK Kwenye Beat afunguka jinsi skendo ya ngono aliyohusika nayo ilivyomwathiri

Muhtasari

•DK amefichua kwamba baada ya skendo hiyo kutokea, alihofia sana kujitokeza hadharani na alikosa watu wa kushirikiana naye katika kipindi hicho kigumu.

•DK amesema kuona alifanikiwa kupata mtoto baada ya madai hayo ni ushahidi tosha  hakuwa na ugonjwa huo wa zinaa.

Image: INSTAGRAM// DK KWENYE BEAT

Mwimbaji wa nyimbo za Injili David Kilonzo almaarufu kama DK Kwenye Beat amekiri kwamba wakati alitajwa kwenye skendo ya ngono ndicho kipindi kigumu zaidi kuwahi pitia maishani.

DK amefichua kwamba baada ya skendo hiyo kutokea, alihofia sana kujitokeza hadharani na alikosa watu wa kushirikiana naye katika kipindi hicho kigumu.

"Huo ni wakati ambao nilikaa miezi sita nyumbani. Sikuwa nafanya chochote, singejitokeza hadharani. Sikuwa na watu wengi wa kushirikiana nao. Ningehesabu watu ambao nilikuwa nao maishani kwa wakati huo," DK alisema akiwa kwenye mahojiano na Diana Marua.

Baba huyo wa mtoto mmoja alikiri haikuwa rahisi kupambana na hali hiyo kwani kwa wakati huo mkewe, Shanice Wangechi, alikuwa nchini Qatar kwa sababu za kikazi.

"Yote yalitendeka nikiwa pekee yangu. Haikuwa rahisi kwangu," Alisema.

Mwaka wa 2019, DK  Kwenye Beat pamoja na mwimbaji mwenzake wa injili Hope Kid walishtumiwa kushirikiana kufanya mapenzi na mwanadada mmoja kutoka Nakuru.

Wanamuziki hao wawili walidaiwa kumwambukiza mwanadada huyo ugonjwa hatari wa zinaa unaotambulika kama Herpes.

DK amesema kuona alifanikiwa kupata mtoto baada ya madai hayo ni ushahidi tosha  hakuwa na ugonjwa huo wa zinaa.

"Watu wakifanya uchunguzi vizuri watajua mtu ako na Herpes ata kupata mtoto ni tatizo. Sikutaka kueleza mtu. Nilijaribu punde baada ya skendo kutokea lakini haikufanya kazi," Alisema.

Mwanamuziki huyo alitangaza kwamba watu wote ambao walihusika na skendo hiyo hawatakuwa na amani kwani aliwaombea sana katika kipindi hicho.