"Singeweza kunywa chai kama sijakunywa pombe!" Omosh afunguka kuhusu uraibu wa pombe

Muhtasari

•Akizungumza katika mahojiano, Omosh alifichua alikuwa amezama kwenye uraibu wa pombe kwa takriban miongo miwili.

•Alisema alifanya uamuzi wa kuenda Rehab mwenyewe baada ya kuona jinsi pombe ilikuwa imemwathiri  vibaya.

Image: INSTAGRAM// OMOSH KIZANGILA MWENYEWE

Mwigizaji Joseph Kinuthia almaarufu Omosh amekiri kuwa jambo analojuta zaidi maishani ni kuwahi kuonja pombe. 

Akizungumza katika mahojiano, Omosh alifichua alikuwa amezama kwenye uraibu wa pombe kwa takriban miongo miwili.

"Majuto yangu makubwa ni kwa nini niliwahi kunywa pombe. Kwa nini niliwahi onja pombe!" Omosh alisema akiwa kwenye mahojiano na Grace Makena.

Omosh alisema uraibu wa pombe ulikuwa umemwathiri kiasi cha kwamba hangeweza  kufanya kazi kama kawaida bila pombe. 

"Nilikuwa mraibu kwa takriban miaka 20. Wakati huo singeweza kula ama kunywa chai asubuhi kama sijachomwa. Asubuhi nikiamka ningetoa sababu yoyote ili nitoke kwa nyumba ndio niende nikakunnywe," Alisema.

Mwigizaji huyo alijaribu kuficha familia kuhusu uraibu wake wa pombe ila hatimaye akapatikana.

Alisema alifanya uamuzi wa kuenda Rehab mwenyewe baada ya kuona jinsi pombe ilikuwa imemwathiri  vibaya.

"Nilianza kunywa kitambo sana. Ilifika wakati nikaona imetosha. Niliona kuwa ile pombe nilikuwa nimekunywa ingemwagwa kwa mtaro, mtoto wa miaka saba angeweza kubebwa nayo. Nilijitolea nikaenda nikaambia dadangu akaniambia tuende Rehab," Alisema.

Omosh alisema baada ya kutoka rehab hakuwahi kuonja mvinyo tena kwa takriban miaka minne. Hata hivyo janga la Corona lilipokumba dunia alijipata kwenye majaribu na kuanza kulewa tena.