Haji Manara awashangza wengi kwa kuoa wake wawili ndani ya miaka 2

Muhtasari

• Haji Manara ametangaza rasmi kwamba ameoa mke wa pili, hii ni kupitia picha alizopakia katika ukurasa wake wa Instagram.

• Aliwashukuru wote waliochangia katika ufanisi wa shughuli hiyo ambayo ilikuwa ya kufana.

Haji Manara na mke wake wa pili katika hafla ya kufunga ndoa
Haji Manara na mke wake wa pili katika hafla ya kufunga ndoa
Image: Instagram

Msemaji wa klabu ya Yanga huko Tanzania, Haji Manara amewashangaza mashabiki wake baada ya kuoa mke wa pili miaka miwili tu baada ya kufunga ndoa na mke wake wa kwanza.

Kupitia picha na ujumbe aliopakia katika ukurasa wake wa Instagram, Manara alisema kwamba haikuwa shughuli rahisi na pia akawashukuru wote ambao kwa namna moja au nyingine walichangia katika ufanisi wa hafla hiyo.

"Haikuwa rahisi lakini kila jambo lina utaratibu wake vile Muumba wetu alivyojaalia," Manara aliandika.

Manara aliwashukuru wazazi wake kwa kuwapa baraka wanapokuwa wanaanza safari hiyo mpya.

Aidha, alimkaribisha mke wake wa pili, Rubynah  Salum katika familia yak huku akiahidi kumlinda na kumtunza kulingana na mila na tamaduni za dini ya kiislamu.

Mastaa mbalimbali walijitokeza kumhongera Manara huku wakimtakia kila la kheri katika ndoa yake na kuwataka waishi kwa amani na upendo.

"Hongera sana, idumu milele," Uncle Shamte aliandika.

"Ikawe kheri inshaallah! Hongera kakaangu," Zamaradi aliandika.

Kuna baadhi ya mashabiki walitoa maoni yao wakisaili iwapo ataweza kuwamudu wake hao wawili, wakisema kwamba Manara anakimbilia kuoa kwa sababu amepata hela.

Ifahamike kwamba katika dini ya Kiislamu, mwanaume anaruhusiwa kuoa wake wanne maadamu tu ana uwezo wa kuwatunza wote kwa usawa.