"JKIA niliitishwa pesa kila sehemu" - Mchekeshaji wa Nigeria Aloma Isaac

Alisema alifikiria hiyo tabia iko Nigeria pekee lakini akaipata hadi Kenya.

Muhtasari

“Hatimaye, uwanja mwingine wa ndege ambapo niliombwa pesa na kunyang'anywa karibu kila sehemu - UWANJA WA NDEGE WA KENYA,” - Aloma Isaac.

Aloma Isaac
Image: Instagram

Mchekeshaji maarufu kutoka Nigeria Ziscaloma almaarufu Aloma Isaac Junior ametuhumu maafisa katika uwanja wa kimataifa wa ndege JKIA nchini Kenya kwamba walijaribu kumtoza pesa nyingi zenye gharama zisizoeleweka.

Kupitia kwa Twitter yake, mchekeshaji huyo alisema kwamba alipoingia nchini Kenya, katika uwanja huo wa JKIA aliitishwa pesa nyingi katika sehemu mbali mbali.

“Hatimaye, uwanja mwingine wa ndege ambapo niliombwa pesa na kunyang'anywa karibu kila sehemu - UWANJA WA NDEGE WA KENYA,” aliandika Aloma Isaac kwenye mtandao wake wa Twitter.

Mchekeshaji huyo aliendelea kusema kwamba hulka kama hiyo alidhani ipo nchini kwao pekee lakini akastaajabu kupata kwaamba hata Kenya maafisa katika uwanja wa ndege wana tabia kama hiyo ya kutafutia mtu makosa na kumlimbikizia.

“Omoh, karibu nilifikiri niko Nigeria. Ikiwa ni mara yako ya kwanza nchini Kenya, jua tu kwamba wanaweza kudanganya chochote ili tu kupata pesa kutoka kwako,” alisema.

Alipotua katika uwanja wa JKIA, Aloma Isaac alikutana na wakuza maudhui Nicholas Kioko na mwenzake Vincent Mboya ambao walizungumza naye kidogo.