"Khaligraph ni mwizi, aliibia Sailors Gang ngoma ya 'Kwenda'" - Lexxy Yung

Lexxy Yung, mmoja wa kundi la Sailors alisema Khaligraph alitumiwa ngoma hiyo aongeze mistari yake iwe collabo lakini akaichukua kabisa.

Muhtasari

• Msanii Lexxy Yung alisema baada ya kuibiwa ngoma na Khaligraph, tukio hilo liliwavunja moyo hadi wakaona sanaa imejaa nyoka.

msanii wa Sailros Gang, Lexxy Yung
Image: Youtube (Screenshot)

Msanii Lexxy Yung ambaye alikuwa mmoja katika kikundi cha Gengetone cha Sailors Gang kilichoteka miaka mitatu iliyopita amezungumza kwa mapana kile kilichosababisha kikundi hicho kusambaratika pamoja na masaibu yaliyowakumba enzi nyota yao iking’aa.

Akizungumza na Lily, mtangazaji anayefanya mahojiano ya wakuza maudhui wa kidigitali nchini kenya, Yung alisema kwamba kando na ubinafsi kusababisha kifo cha Sailors Gang, bali pia walikumbwa na changamoto kama kuibiwa ngoma na baadhi ya wasanii maarufu nchini.

Alipoulizwa kama kuna collabo walifanya na hazikutoka kwa sababu moja au nyingine, Yung alisema ndio na hadi kuwataja baadhi ya wasanii walioshirikiana nao akiwemo DNA na Kahligraph Jones ambaye alisema aliwaibia wimbo.

“Khaligraph Jones ni mwizi. Kuna vile alitumiwa ngoma yetu na akaifanya yake. Nadhani hivyo ndivyo anavyowafanyia wasanii wengi wanaochipukia ambapo anatumiwa wimbo kuskiza ili kufanya collabo, anaufanya wake,” Lexxy Yung alisema.

Alipoulizwa ataje ni ngoma gani Khaligraph Jones aliwaibia, msanii huyo alisema kwamba mfalme huyo wa kurap aliwaibia ngoma kwa jina la ‘Kwenda’

“Tulienda kwa studio ya BMR tukawa na Kashkid na akatuambia Khaligraph anataka ngoma, kila mtu akaingia kazi kufanya kipande chake. Tukasikilizana na kutengeneza ngoma inaitwa ‘Kwenda’ na hadi tuko na ngoma asili. Tukamtumia ngoma aweke verse, akaweka na mpaka video na kuipakia kwenye mitandao,” Yung alisema.

Msanii huyo alisema kwamba tukio hilo liliuma kila mtu katika kundi la Sailors mpaka wakakufa moyo kabisa ambapo walikuwa wanaona kila mtu katika Sanaa sasa ni kama nyoka.

“Tukio hilo liliuma kila mtu kwa Gang mpaka tukawa tunaona sanaa imejaa nyoka. Sailors ndio hawa wametoa ngoma halafu tunazungukwa, sasa tukaona Sanaa si yetu tena ndio tukagawanyika,” Lexxy Yung alielezea kwa sikitiko kubwa.

Alisema kwamba shida kubwa ni wao kwa sababu baada ya masaibu kuwakumba walipokosana na mfadhili wao mkubwa, mtangazaji Mwalimu Rachel, kila mtu aliamua kukimbia na kuanza kujijenga maisha kivyake badala ya kujumuika kutafuta mbinu mbadala ya kubaki kwenye Sanaa.