Ringtone: Rungu ya Alai ilinivuruga akili, nililia kutekeleza wajibu kama mtoto wa Mungu

Kwac mara ya kwanza msanii Ringtone amezungumzia madhara rungu ya mwanablogu Alai ilimsababishia.

Muhtasari

• "Nililia ili kutumia hazina ya machozi ambayo Mungu aliniwekea, nilikuwepo sijalia muda mrefu,” - Ringtone

Aliyekuwa mwenyekiti wa wasanii wa injili Kenya
Aliyekuwa mwenyekiti wa wasanii wa injili Kenya
Image: Ringtone Apoko (Instagram)

Baada ya video ya msanii Ringtone Apoko akilia mahakamani kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii, hatimaye msanii huyo amelizungumzia tukio hilo ambalo wengi waliligeuza kuwa kioja cha kuchekesha kwa jinsi alivyokuwa akitokwa na machozi kwa kwikwi huku akielezea hakimu kilichotokea.

Ringtone alikuwa mahakamani akielezea kilichotokea baina yake na mwanablogu Robert Alai ambaye alimpiga rungu moja kichwani baada ya mzozo wa magari yao kukwaruzana kwenye barabara moja katika mtaa wa kifahari wa Kilimani, mwishoni mwa mwaka jana.

Ringtone alitetea kitendo chake cha kulia na kusema kwamba mtoto wa kiume pia ana haki ya kulia na ilikuwa haki yake ya kutekeleza wajibu wa maana ya machozi.

“Kwani mwanaume hafai kulia? Nililia kwa sababu unajua wakati mwingine watu wanafikiria mimi si binadamu. Kwa kulia kwangu nilihimiza watoto wa kiume kwamba ukisikia kulia, lia tu kwa sababu Mungu angekuwa amepangia wanaume wasilie hangewawekea machozi. Kwa hiyo mimi nilikuwa natekeleza wajibu wangu wa kulia kama mtoto wa Mungu, na pia kutumia hazina ya machozi ambayo Mungu aliniwekea, nilikuwepo sijalia muda mrefu,” alieleza Ringtone.

Vile vile msanii huyo kwa kiduchu alipata kuzungumzia madhara lile rungu la kichwani lilimsababishia kiafya ambapo alisema wakati mwingine tangu kupigwa huwa akili yake inapata matatizo ya kupoteza kumbukumbu.

“Nishapona lakini akili yangu bado, wakati mwingine huwa nakuwa na upoteaji wa kumbukumbu, wakati mwingine kichwa kinauma sana, yaani kwa kifupi kichwa changu kiko na shida tangu yule mwanaume anigonge bila sababu na bila hatia,” alielezea Ringtone.