Maoni: Utajiri wa Diamond umetokana na mafanikio ya Harmonize na Rayvanny kimuziki

Harmonize aliondoka WCB miaka 3 iliyopita naye Rayvanny ametangaza kuondoka jana

Muhtasari

• Katika kila mradi wa kazi ya muziki ambayo wasanii hao walikuwa wanafanya, lebo ya wasafi ilikuwa ikivuna asilimia hata kubwa kuliko ile inaendea mwenye ngoma.

• Harmonize aliwahi fichua kwamba alikuwa anapata 40% na lebo kuchukua 60% ya mapato yote kimuziki.

Wasanii wqa bongo fleva, Harmonize, Diamond Platnumz na Rayvanny
Wasanii wqa bongo fleva, Harmonize, Diamond Platnumz na Rayvanny
Image: Instagram

Baada ya msanii Rayvanny kuweka wazi kwamba muda wake umekamilika kuitumikia lebo ya Wasafi ambayo kinara wake ni Diamond, sasa wadau mbalimbali katika fani ya muziki wa bongo fleva wamejitosa mezani kulijadili hilo kwa undani na athari za wasanii wakubwa kama hao kuondoka WCB.

Mdau mmoja kwa jina Hopeman David ameachia ujumbe mrefu akilichanganua suala la wasanii wakubwa kuigura lebo hiyo inayosemekana kuwa kubwa kabisa katika ukanda wa Afrika mashariki.

Ikumbukwe alianza kuondoka Rich Mavoko baada ya kusemekana kwamba alikuwa chini ya shinikizo kutoa muziki na michongo mingine ya kichini chini, akaja akafuata Harmonize ambaye kuondoka kwake kulikuwa kama pigo kubwa kwa msanii Diamond ambaye kwa wakati mmoja aliwahi kiri hadharani kwamba Harmonize ndiye msanii aliyekuwa na riziki kubwa katika wasanii wote ndani ya WCB.

Sasa Hopeman David ameachia maoni akisema kwamba mafanikio makubwa ya utajiri wa Diamond katika miaka kama 7 iliyopita yametokana na jitihada za wasanii Rayvanny na Harmonize.

“Hivi sasa Diamond anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dollar million 7. Miongoni mwa Biashara kubwa zilizochangia utajiri huo katika Lebo yake. Wasafi imemuingizia pesa nyingi sana kutoka kwenye makato ya wasanii wake. Mfano Harmonize alikuwa kila anachoingiza pale WCB anapewa Asilimia 40, kisha 60 zinaenda kwa Diamond. Imagine Harmonize amekaa pale zaidi ya miaka minne, unahisi Diamond alivuna kiasi gani cha pesa?” aliuliza mshikadau huyo.

Alisema pia kwa miaka 6 ya Rayvanny chini ya uongozi wa WCB Diamond alivuna pakubwa kutokana na kazi zake zilizofurahikiwa sana mpaka kuwa msanii wa kwanza kutoka Afrika mashariki kufikisha streams milioni 100 kwenye jukwaa la Boomplay miongoni mwa rekodi nyingine nyingi alizoziandikisha.

“Tuachane na Mavoko, Queen Darlin na LavaLava hawa sidhani kama Diamond ameingiza pesa ya maana kupitia wao. Ila ZUCHU, HARMONIZE NA RAYVANNY nina uhakika ameingiza pesa nyingi sana kupitia wao,” alisema Hopeman.

Msau huyo alidai kwamba Diamond alikuwa akiwajenga ndio lakini kwa kuwapandilia mgongoni na kufaidi mara mbili zaidi yao na hivyo kuwataka pia wafanye hivo ili kuishi maisha mazuri.

“Cha muhimu sana, Harmonize na Rayvanny inabidi watafute vijana wa kuwapandia mgongoni kama ambavyo wao walipandiwa na Diamond Platnumz. Kwa kufanya hivyo Watawasaidia vijana pia wao watafaidika mara mbili zaidi,” alimwaga maoni.