Cartoon Comedian afunguka kukumbwa na msongo wa mawazo

Amefichua kuwa amepoteza marafiki wengi katika kipindi ambacho amekuwa akipambana na hali hiyo.

Muhtasari

•Cartoon Comedian amekiri kuwa amekuwa akipambana na msongo wa mawazo kwa kipindi kisichothibitishwa mwaka huu.

•Pia alifichua kuwa amepoteza marafiki wengi katika kipindi ambacho amekuwa akipambana na hali hiyo.

Image: INSTAGRAM// CARTOON COMEDIAN

Mchekeshaji Vanessa Akinyi almaarufu Cartoon Comedian amekiri kuwa mwaka wa 2022 haujakuwa rahisi kwake.

Akizungumza kupitia ukurasa wake wa Instagram, Cartoon alifunguka kuwa  mwaka huu amekuwa akipambana na msongo wa mawazo. 

"2022 niliingia kwenye msongo wa mawazo," Cartoon alisema kupitia Instastori zake.

Mchekeshaji huyo aliambatanisha chapisho lake na wimbo wa mandharinyuma ulioashiria kuwa huenda  yuko pweke.

"Maana nilihisi kila kitu, Lakini hakuna anayesikiliza, Na hiyo ni upweke tu. Nina upweke sana," Yalisema maneno ya wimbo huo.

Cartoon pia alifichua kuwa amepoteza marafiki wengi katika kipindi ambacho amekuwa akipambana na hali hiyo.

"Nilipoteza watu wengine njiani lakini sasa hivi mniruhusu niwaambie kuwa kila kitu kitakuwa sawa," Alisema.

Msanii huyo hata hivyo amekuwa akiwaburudisha mashabiki wake kupitia video za kuchekesha licha ya kukabiliwa na msongo wa mawazo.

Msongo wa mawazo umekuwa hali ya kawaida miongoni mwa wasanii wengi hasa wale wenye umri wa ujana.

Ni suala ambalo linafaa kuangaziwa kwa umakini kwa kuwa umefanya wasanii wengi kupoteza mwelekeo wa maisha, kuzama kwenye uraibu wa dawa za kulevya, kufilisika miongoni mwa athari zingine za kutisha.

Takriban miezi miwili iliyopita mchekeshaji Flaqo alijitokeza kufichua kuwa alikosekana kwenye sanaa kwa kipindi kirefu baada ya kukabiliwa na matatizo ya afya ya akili.

Flaqo alieleza  kuwa licha ya umaarufu mkubwa ambao amejizolea tayari hakuwa na furaha sana.

"Nakumbuka nilimaliza shoot, nalikuwa na hisia fulani, Bien anajua haya, nilimpogia Bien simu nikaanza kusema mambo hata hayana maana,alinipa namba ya simu ya mtaalamu, ilikuwa hisia fulani sijui niseme Bipolar au Depression, nimekuwa nikipigana na hayo kwa mwaka mmoja sasa," Flaqo alisema.

Mchekesahaji huyo alisema safari ya kupata afueni na kurejelea hali ya kawaida haijakuwa rahisi kwake.

Flaqo pia alifichua kuwa amekuwa akitembelea mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia kwa kipindi cha  mwaka mmoja ambacho kimepita na kuweka wazi kuwa sasa yupo sawa.