Irene Uwoya: Ukishindwa na mapenzi jaribu kilimo ndugu yangu utanishukuru baadae

Irene Uwoya alisema hakuna haja kujing'ang'aniza katika mapenzi bila faida hali ya kuwa fani ya kilimo kuna manufaa mengi.

Muhtasari

• “Nimeshajaribu vyote nimeshindwa sasa hivi sijui nifanyeje?” mmoja kwa jina Dullah Tameer alitaka kuelezewa zaidi.

Muigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Irene Uwoya
Muigizaji mkongwe wa Bongo Movie, Irene Uwoya
Image: Instagram//IreneUwoya8

Muigizaji mkongwe ambaye bado ni pisi kali kutoka Tanzania, Irene Uwoya amekuja na jipya baada ya kudai kwamba watu wengi katika karne hii ya sasa wanateseka na mapenzi na hivyo kuwataka wale wote wanaojihusisha na mapenzi iwapo watashindwa kwenye kitivo hicho basi wajaribu bahati yao katika kilimo, pengine huko ndiko shani yao ipo.

Kulingana na Uwoya, haina haja mtu kujining’iniza kweney mapenzi bure na majibu yake ni kuumizwa kutwa kucha kubutuliwa dumu la kombolela la moyo hali ya kuwa bahati na furaha yako iko katika fani ya ukulima. Alisema yeyote atakayefanya udhubutu wa kujaribu kufuata ushauri wake basi atakuja kumshukuru mbeleni.

“Ukishindwa na mapenzi jaribu kilimo ndugu yangu …utanishukuru baadae,” aliandika Uwoya kwenye Instagram yake.

Maneno haya ya Uwoya yalipokelewa kwa njia mseto huku baadhi wakisema kwamba kuna wale wamejaribu vyote na tayari wameshindwa na kutaka ushauri zaidi kupewa jaribio la fani ya tatu kando na kilimo na mapenzi.

“Nimeshajaribu vyote nimeshindwa sasa hivi sijui nifanyeje?” mmoja kwa jina Dullah Tameer aliandika.

Muigizaji huyo mkongwe ambaye pia ni mama ni mmoja wa watu maarufu wasiokuwa na bahati kwenye mapenzi kwani amejaribu sana kumpata mwenza ila mpaka sasa bado bahati haijasimama. Wengine walitumia kigezo hiki kumuuliza kwa kuwa yeye ametendwa sana katika mapenzi ana mashamba mangapi iwapo aliamua kujaribu kilimo.

“Una mashamba mangapi mpaka sasa? Maana wewe ni mfano hai ya waliokucheka kwenye mapenzi,” mwingine alitoa maoni.

Uwoya katika siku za hivi karibuni ameonekana kutolea ushauri komavu kwa mashabiki zake tangu wiki chache zilizopita aalikwe kwenye sherehe ya kanisa kama mgeni maalum katika ibada ya kusherehekea miaka minane tangu kanisa moja mjini Morogoro kuanza kutoa huduma ya uponyaji na mahubiri.