Sijawahi kumtusi Diamond, Lokole anabweka uongo - Lukamba

"Unanikanda eti sina fadhila, wewe unajuaje,” Lukamba alifoka.

Muhtasari

• "Wewe kama mtangazaji wa Wasafi FM au Wasafi TV, hauna mamlaka ya kunizungumzia mimi" - Lukamba alimwambia Lokole

Mfanyikazi huyo wa zamani amekanusha kumtukana Diamond aliyekuwa bosi wake
Lukamba, Diamond Mfanyikazi huyo wa zamani amekanusha kumtukana Diamond aliyekuwa bosi wake
Image: Instagram

Msanii mpya kabisa kwenye tasnia ya muziki wa Bongo Fleva, Lukamba ameamua kuvunja ukimya wake kuhusu mambo yanayoendelezwa haswa na watangazaji wa Wasafi kusema kwamab yeye baada ya kutoka Wasafi ameanza kumtusi aliyekuwa bosi wake Diamond Platnumz.

Juzi kati baada ya kutoa wimbo wenye utata aliowataja wasanii wote waliotoka Wasafi pamoja na pia kumtaja Diamond, watangazaji kama vile mchambaji Juma Lokole walikunja mashati na kumkujia juu kwamba ameanza kumdhalilisha Diamond na hana fadhila.

Lukamba amelizungumzia suala hilo kwa undani na kujitetea vikali kwamba watu walioko kwenye vituo vya Wasafi TV na Redio hawana haki ya kumzungumzia yeye kwa sababu yeye hakuwa upande wa redio au runinga.

Alisema watu wanaofaa kumzungumzia ni wale wanaosimamia lebo ya Wasafi kwa sababu hicho ndicho kitengo alikokuwa akifanya kazi.

Alisema watangazaji licha ya kuwa chini ya bosi mmoja lakini hawafai kumzungumzia kwa mitikasi yake ya kimuziki kwani Sanaa ni kibwa na kuipa ladha kuna baadhi na maneno msanii anayatunga na majina ya watu ili kuoanisha vina katika mishororo kuleta ladha ya ushairi.

“Mimi ni msanii, wewe kama mtangazaji wa Wasafi FM au Wasafi TV, hauna mamlaka ya kunizungumzia mimi kwenye lebo ya Wasafi. Usikuje kutoa siri zangu kwenye TV wakati wewe si mtu wa lebo. Mimi sijamtukana Diamond kwenye wimbo wangu. Unanikanda eti sina fadhila, wewe unajuaje,” Lukamba alifoka.

Alimuingilia chawa wa Diamond, mtangazaji mchambaji Juma Lokole kwa kusema kwamab huyo ndiye yupo mstari wa mbele kumkandia kwamba hana fadhila kwa Diamond baada ya kumtoa sasa ameanza kumkejeli kwenye nyimbo.

Lukamba alisema kwamba Lokole kwanza yeye ni mchambaji na hana kitu chochote katika taaluma ya utangazaji kazi yake ni kubweka tu kwa sababu alionekana kubweka kumtetea Diamond ndio maana alipatiwa kazi.

“Mtu kama Juma Lokole, kwanza taaluma ya Utangazaji hana, yaani yeye alikuwa anachamba, akaonekana ana wafuasi wengi, akaitwa njoo kaa hapa, lakini tuseme taasisi zianze kufuatilia kwamba zinawaajiri watu kutokana na taaluma basi Juma Lokole nje!” Lukamba alimwaga mtama kwenye kuku wengi.