Lilian Ng'ang'a afunguka kuhusu harusi yake na Juliani

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema kuwa harusi hiyo ilikuwa ya siri na ya faragha.

Muhtasari

•Juliani alifunga pingu za maisha katika hafla ya siri ya iliyofanyika jijini Nairobi mwezi Februari mnamo siku yake ya kuzaliwa.

•Lilian alisema maisha yao ya ndoa yamekuwa rahisi.

Lilian Ng'ang'a
Image: Caroline Mbusa

Aliyekuwa mama wa kaunti ya Machakos Lilian Ng’ang’a amefunguka kuhusu harusi yake ya siri na mume wake Julius Owino almaarufu Juliani.

Mama huyo wa mtoto mmoja alifunga pingu za maisha katika hafla ya siri ya iliyofanyika jijini Nairobi mwezi Februari mnamo siku yake ya kuzaliwa .

Picha za harusi yao hazikusambaa sana kwani picha moja tu ndiyo iliyoweza kupenyeza kwenye mitandao ya kijamii.

Lilian alikuwa amevalia gauni la rangi ya waridi lililokuwa limebubujika hadi chini na mume wake Juliani alikuwa amevalia shati nyeupe-theluji na koti ya pembe, suruali nyeusi  na viatu vyeupe.

Juliani alikuwa na wasimamizi watatu,huku Ng’ang’a akiwa na wasimamizi wawili wa kike waliovalia gauni za lavender za bega.

Mandhari ya harusi hiyo yalikuwa rangi nyeupe na nyeusi na wanandoa hao waliweza kuwaalika watu chini ya 50.

Akizungumza na Mpasho, Lilian alisema kuwa harusi hiyo ilikuwa ya kibinafsi na ya faragha.

Hakukuwa na mengi ya kupanga kwa hivyo haikutuchukua muda kupanga harusi hiyo, ilichukua muda wa miezi miwili pekee,”alisema.

Alisema picha iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii ilikuwa ya watu waliokuwa wakijiburudisha kwenye mazingira ya harusi yao na kuwa alitamani kuwa watu hao wangeiheshimu faragha yake.

“Hayo yalikuwa makosa, harusi ilikuwa ya faragha, ilipaswa kuwa binafsi. Kwa yule aliyeona haki ama haja ya kuanika picha hiyo, ilikuwa makosa. Lakini kila kitu hutendeka na sababu yake,”alisema.

Lilian alieleza kuwa harusi hiyo ilikuwa hafla ya kawaida tu na ndio lililoifanya iwe ya kupendeza. “Ni miongoni mwa siku bora zaidi kwa mwaka katika maisha yangu,”alisema.

Alipoulizwa kama walienda kwa honeymoon yoyote ile, mpenzi huyo wa Juliani alisema kuwa honeymoon yao huwa kila siku.

Usifanye harusi kisha uende kwenye fungate ya siku moja. Kuwa na uzoefu wa kuwa kwenye fungate kila siku. Tuko kwenye fungate bado ila tulizuru Kenya wakati huo,”alisema.

Alisema viapo vya Juliani vilikuwa vyenye kina sana na hilo ndilo lililojitokeza na kuwa la pekee wakati wa harusi yao.

Ni mtu mbunifu sana, na maneno yake yaliniteka.Yalikuwa ya kupendeza sana,”alisema.

Alipoelezea kuhusu maisha yake ya ndoa na Juliani kwa mwaka sasa, Lilian alisema maisha yao yamekuwa rahisi.

Mapenzi yanafaa kuwa hivyo. Yanafaa kuwa rahisi kama kupumua. Naipenda kwa sababu huyu ni mtu anayenitakia mema miongoni mwa mambo mengine,” Ng’ang’a alisema.

Juliani na Lilian walitangaza uhusiano wao wa kimapenzi wiki chache baada ya Lilian kuweka kikomo kwenye uhusiano wake na aliyekuwa mchumba wake, Gavana Alfred Mutua mwaka wa 2021.