Kutoka wakati ambao nilijua nimekubeba, nilikupenda - Wahu amwandikia bintiye Shiru

Hii ni baada ya kuwa na muungano wake wa kwanza na bintiye baada ya kujifungua

Muhtasari

• Wahu amemwandikia binti yake ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram, ujumbe ambao umewatoa wengi chozi la furaha kwa uzuri wake.

• Mpenzi huyo wa Nameless alisema kuwa alimthamini mwanawe na kumwonyesha mahaba ya kuwa na hamu kumtarajia alipokuwa na uja uzito.

Wahu// Nameless

Wanamuziki Wahu na Nameless walimkaribisha mtoto wao wa kike jana Jumanne wakiwa wamejawa na furaha.

Wahu amemwandikia binti yake ujumbe kwenye ukurasa wake wa Instagram, ujumbe ambao umewatoa wengi chozi la furaha kwa uzuri wake.

Wanamuziki hao waliwashukuru wote ambao wamewaunga mkono na kuwa nao wakati huo wa uja uzito.

Mama huyo wa watoto watatu sasa alieleza hisia zake alipokuwa na uja uzito wa bintiye mpaka sasa ambapo amejifungua.

Wahu alichapisha video iliyoonyesha akipewa mwanawe kwa mara ya kwanza baada ya kujifungua. Alitoa machozi ya furaha huku akimkumbatia bintiye Shiru.

Mpenzi huyo wa Nameless alisema kuwa alimthamini mwanawe na kumwonyesha mahaba ya kuwa na hamu kumtarajia alipokuwa na uja uzito.

"Kutoka wakati ambao nilijua nimekubeba, nilikupenda. Nilipenda kukuhisi ukiwa tumboni mwangu, ukigeuka na nilipokuwa nikienda kliniki kuona madaktari na kuskia mpigo wa moyo wako," alisema mama huyo.

Wahu aliongeza kuwa alipenda kuwa na ukaribu na bintiye kwa kuwasiliana kwa njia tofauti naye alipokuwa na uja uzito.

Alisema kuwa alikuwa na matukio ya hisia tofauti ila alipenda na kumtarajia Shiru kwa hamu kwa muda huo wote aliobeba uja uzito wake.

"Nilikuwa napenda kukuimbia na kukuongelesha. Nilikuwa na wasisiwasi nilipokuwa nikikungoja, nimeomba na nilikuwa na hisia chungu nzima kwa miezi 9 iliyopita, ila sasa tupo hapa," Wahu alisema kwenye chapisho lake la Instagram.

Alieleza muunganisho wake na Shiru kwa mara ya kwanza na kusema kuwa ulikuwa muda wa hisia tofauti ila amejawa na furaha tele.

"Nilipokubeba kwenye mikono yangu hatimaye, siwezi kueleza kilichokuwa kinaendelea wakati huo. Ninachoweza kusema ni Asante Mungu, umetuonekania mpaka sasa," Wahu alimwandikia bintiye Shiru.

Nameless alichapisha picha ya muunganisho huo wa Wahu na bintiye Shiru huku akionyesha sura ya binti yake.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa siku hiyo ilikuwa siku maalum kwao na familia yao kwa ujumla.

"Muunganiko wa kwanza wa mama na Shiru, tunawashukuru wote kwa ujumbe mliotutumia za hongera na kututakia mema," Nameless alisema huku akiwatakia mke wake na binti yake usiku mwema.