Vera Sidika awafokea wanamitandao wanakejeli nywele za bintiye Asia

Sidika hakufurahishwa na wanamitandao waliomkemea kwa kusema nywele alizobandikwa Asia ni nzito

Muhtasari

• Sidika alikuwa amesukwa nywele ambazo pia bintiye Asia alikuwa amesukwa nazo kwa minajili ya kupigwa picha za kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa bintiye.

• Mwanasosholaiti huyo alisema kuwa anafahamu kilicho bora kwa bintiye.

Bintiye Vera Sidika na Brown Mauzo, Asia

Mwanasosholaiti Vera Sidika aliwafokea wanamitandao waliomsema binti yake, Asia Brown kwa nywele alizokuwa amesukwa.

Vera alikuwa ametafuta fundi wa nywele kumtengeneza mwanawe kwa minajili ya kupiga picha za kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwa mtoto huyo wake.

Alisema kuwa wanamitandao wengine walitoa maoni kuhusu nywele za mwanawe, maoni ambayo hayakumfurahisha.

Kulingana na alichosema Vera, wanamitandao hao walikuwa wamekejeli nywele za bintiye na kumkemea Vera kwa kumsuka kwa nywele nzito.

"Lakini ushamba ni mbaya, watu ambao wameweza kujaribu aina za nywele wanaweza kukuambia kuwa aina hii ya Marley Braids ni nyepesi sana kama mbawa," mama huyo wa mtoto mmoja alisema.

Vera alisema kuwa anampenda bintiye sana na kuwa hawezi kumfanyia jambo ambalo anajua halitamfurahisha.

Aliwafokea wanamitandao hao kwa kumkemea na kuwashauri wajaribu aina nyingine za nywele kabla ya kukejeli wasichoelewa.

Alieleza sababu yake ya kumsuka bintiye nywele hizo na kusema kuwa yeye ndiye atakayeamua cha kumfanyia.

"Namthamini binti yangu sana, siwezi kumsuka kitu nzito au kitakachomdhuru kwa hivyo kabla ya kuja kunihukumu mfanye ukaguzi wenu kwanza. Tulikuwa tunafaa kufanana na binti yangu na hiyo ndiyo ilikuwa njia bora zaidi ili iendane na nguo tulizochagua," mwanasosholaiti huyo alieleza sababu yake.

Vera alieleza jinsi binti yake Asia hupenda kuwa mtulivu anapotengenezwa nywele ama katika suala lolote la urembo.

Alisema kuwa yeye kama mama ya Asia, ndiye atakayeamua cha kumfanyia bintiye hata watu waseme nini.

"Asia alikaa na nywele hizo kwa saa moja au mbili na baadaye zikatolewa. Lakini watu hupenda kuwahukumu watu na kuwa na fikra hasi. Ni kama mama aliyemzaa mtoto huyo hajui kilicho bora kwake," mama huyo alijitetea.

Jana Alhamisi, Vera alikuwa anasherehekea siku ya kuzaliwa ya binti yake Asia.