Masanja amnunulia mkewe gari licha ya skendo ya kuchepuka na katibu wa kanisa

Wiki chache zilizopita, skendo ya mke wa mchungaji kudaiwa kutoka kimapenzi na katibu wa kanisa aliyejiua ilisambaa mitandaoni.

Muhtasari

• Watu walisema kitendo cha Masanja kumzawidi mkewe gari licha ya uvumi wa kumsaliti kimapenzi ni kama kuwaziba midomo wambea.

Masanja amnunulia mkewe gari licha ya sintofahamu ya kuchepuka
Masanja amnunulia mkewe gari licha ya sintofahamu ya kuchepuka
Image: Instagram

Takribani mwezi mmoja tangu skendo ya mke wa mchungaji Masanja Mkandamizaji kutoka kimapenzi na katibu wa kanisa lao ambaye alijitoa uhai, mchungaji huyo sasa amemsherehekea mkewe katika siku yake ya kuzaliwa kwa zawadi maalum.

Mchungaji huyo baada ya kumalizika kwa ibada ya Jumapili katika kanisa lake la Feel Free, alimfanyia mkewe bonge la shtukizi kwa kumzawadia gari dogo kama njia moja ya kumuonesha upendo wake akisherehekea kuongeza mwaka mmoja katika kapu la maisha yake.

“Heri njema ya siku ya kuzaliwa mke wangu mzuri Msukuma wa Baba. Mungu akutunze, wewe ni mama bora kwa watoto wetu. Japo ni zawadi ndogo lakini kwa sasa ipokee mke wangu,” Mchungaji huyo ambaye pia alikuwa mchekeshaji awali aliandika kweney picha hizo akionekana kumkabidhi ufunguo wa gari hilo.

Itakumbukwa katibu wa kanisa la Masanja alijitoa uhai na kuacha barua ndefu iliyoeleza mapenzi yake kwa mke wa mchungaji huyo huku akisema mapenzi yake ndio chanzo cha kujitoa uhai kwani hangeweza kustahilimi kumuona akikatiza kanisani na baba mchungaji hali ya kuwa moyo wake ulikuwa umelowa kwake.

Baada ya tukio hilo lililochukua mitazamo changamano, mchungaji Masanja Mkandamizaji alivunja ukimya kwa kusema kwamba liwake jua, inyeshe mvua, hakuwa tayari hata kidogo kumuacha mke wake kwa sababu tu ya skendo hiyo.

Kwa maneno yake, Masanja alimhakikishia mkewe upendo na kusimama na yeye muda wake wakati zogo hilo likiendelea kuteketeza wasifu wake kwenye mitandao ya kijamii.

Alisema kwamba hata ndoa ziishe leo na kesho wanaume waamrishwe kuoa upya basi yeye yuko radhi kumrukia mke wake yule yule, huku akiwapasha watu kwamba siku hizi wanapenda sana kutumia nguvu nyingi katika kufuatilia umbea unaolenga kuwaharibia watu.

Tukio la kumzawidi mkewe gari limetajwa na wengi kuwa kitendo kilicholenga kuwa nyamazisha kabisa wambea wanafiki waliokuwa muda wote wakiomba zogo lao kuchukua mkondo wa kutengana na pengine kuanza kurushiana cheche mitandaoni kwa faida ya wanablogu wa udaku.

Ama kweli hapa baba mchungaji amewafunga goli la ushindi wambea!