Janet Mbugua amwandikia mwanawe ujumbe mtamu kwa kufisha miaka 7

Janet Mbugua alikuwa anasherehekea siku ya kuzaliwa ya mwanawe

Muhtasari

• Janet Mbugua alimshrehekea mwanawe Huru Ndichu kwa ujumbe huo alioeleza jinsi safari yake ya ulezi ulivyokuwa.

Janet Mbugua

Aliyekuwa mwanahabari, Janet Mbugua amemwandikia mwanawe, Huru Ndichu ujumbe mtamu huku akisherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Katika mtandao wa kijamii wa Instagram, Mbugua alikumbuka safari ya kumlea mwanawe kutoka pale alipokuwa mchanga hadi sasa ambapo amefikisha miaka 7.

Alimshukuru Mungu kwa kumpa uwezo wa kuwa mama ya watoto wake wawili ambao wote ni wakubwa sasa.

"Wakati mmoja unawakumbatia na kuwabeba kama wachanga waliozaliwa, wakati mwengine wanakaribia kutoshana nawe. Heri ya kuzaliwa unapofikisha miaka 7. Kweli wakati ulienda wapi? Tunakupenda sana mwanangu," Mbugua aliandika.

Alizungumzia urefu wa Huru ambaye karibu anamfikia na kusema kuwa mtoto huyo amerithi urefu wa baba yake.

Mbugua alieleza jinsi amekuwa akijikaza kisabuni kuhakikisha amewapa wanawe mahitaji yao na kuwa wako sawa.

Alisema kuwa kuwalea wanawe wawili limekuwa jambo ambalo angetaka kurudia kufanya kwa kuwa alipenda safari hiyo.

"Nimekuwa nikiwasikia wazazi wengine wakimshukuru Mungu kwa kuwalinda watoto wao mpaka walipo na sasa naelewa kwa sababu najihisi kuheshimika na mwenye baraka tele  kuwaona wakiwa wakubwa. Hata kama mara nusu ya wakati huo huwa hujui unachofanya,  fanya jukumu lako kwa ubora zaidi, kila wakati," mama huyo alieleza.

Alijivunia kuwa mama ya watoto wawili wa jinsia moja ya kiume na hata kujibandika jina chini ya alama ya reli #mamawavulana.

Katika picha aliyopakia Instagram kumsherehekea mwanawe mama huyo wa watoto wawili alikuwa anatembea na watoto wake akiwa amewashika mkono.

"Sasa nalea watoto wawili, mmoja mwenye miaka 4 na mwengine mwenye miaka 7, " Mbugua alisema.