Kate Actress afichua kwa nini hawezi kuhudhuria hafla bila kulipwa

Kate alisema kuwa yeye hutumia zaidi ya laki moja kwa mavazi ya hafla.

Muhtasari

• Alisema kuwa sababu yake si kiburi kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu na kusema kuwa yeye hutumia zaidi ya laki moja kwa mavazi ya kuhudhuria hafla.

• Kate alisema kuwa huwa anahisi vibaya watu wakikosoa mitindo y  watu maarufu wanapohudhuria hafla.

Kate Actress
Image: Kate Actress Instagram

Aliyekuwa muigizaji wa kipindi cha Mother-in -Law, Kate Actress amefichua sababu ya kukataa kuhudhuria hafla isiyo na malipo.

Katika mahojiano na Mungai Eve, Alisema kuwa sababu yake si kiburi kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu na kusema kuwa yeye hutumia zaidi ya laki moja kwa mavazi ya kuhudhuria hafla.

 Kate alisema kuwa mtindo wake wa mavazi wakati akihudhuria hafla huwa haujapangwa wakati mwingine.

Alizungumzia hafla ya hivi majuzi ya Wakanda Premier ambapo mtindo wake wa mavazi uliwafurahisha Wakenya wengi.

"Lazima uvae kulingana na sifa zako, sio mwili wako tu, pata fundi anayekuelewa kama mtu na sifa zako. Mimi na fundi wangu tulipata mtindo huo siku tatu kabla ya hafla hiyo," muigizaji huyo alisema.

Alieleza kuwa matayirisho yake kabla yakuhudhuria hafla; kuanzia na mavazi, nywele, urembo, viatu na hata malipo ya fundi wa nguo huwa ghali.

Mama huyo wa watoto wawili alisema kuwa huwa anahisi vibaya watu wakikosoa mitindo y  watu maarufu wanapohudhuria hafla.

"Sikuanza kama nilivyo sasa, ilinichukua muda. Tuwape moyo watu maarufu. Hata hivyo, wewe unayehudhuria hafla hiyo, jipange mapema, tafuta fundi anayekuelewa mapema ili mbuni kitu. Si lazima kitu kiwe ghali ili uonekane," alisema.

Alisema kuwa kujipanga kwa wakati wa mwisho pia huongeza gharama ya vitu ambavyo vinahitajika ili kuhudhuria hafla.

Muigizaji huyo aliongeza kuwa msukumo wake wa kutia bidii ni kuwa ana majukumu yanayofaa kulipiwa na pia ni jambo ambalo anapenda kufanya.

Hivi majuzi, alibainisha kuwa bado maisha yanampa changamoto ila sasa anaweza kukidhi mahitaji yake mengi na familia yake.

"Wakati maisha yalikuwa yananishughulikia, usichanganyikiwe bado hayako sambamba ila sasa naweza kununua mvinyo mzuri," Kate alisema huku akiwatakia wanamitandao na mashabiki wake siku njema ya Utamaduni.