Huddah akiwasha mitandaoni akijitambulisha kama mama na mke wa mtu

Wengi walipinga kwa kusema kuwa Huddah kwa muda mrefu amekuwa akionesha chuki kwa ndoa na pia katika kupata watoto.

Muhtasari

• Wengine walimtetea kuwa huenda aliasili mtoto kitambo bila mtu yeyote kujua.

• Huddah hajakuwa akipakia maendeleo ya maisha yake mitandaoni zaidi ya kutangaza biashara yake tu.

 

Huddah awashauri kina dada kukaa mbali na wanaume watoto wa mama
Huddah awashauri kina dada kukaa mbali na wanaume watoto wa mama
Image: Instagram

Mwanasosholaiti wa muda mrefu Huddah Monroe amezua mkanganyiko kwenye mitandao ya kijamii baada ya kujitambulisha upya akijiita mke na mke wa mtu.

Kupitia instastory yake, Mjasiriamali huyo wa bidhaa za kujipodoa alipakia picha yake akiwa na muonekano mpya ambapo kwa mara ya kwanza alionekana amefunga kitambaa kichwani na kuvalia nguo zilizositiri sehemu kubwa ya mwili wake kinyume na mavazi yake ya kawaida ambayo ni ya kutongoza na kuvutia macho ya wanaume wengi.

Alisema kuwa yeye kando na kuwa binti wa mtu na mfanyibiashara mkubwa, pia ni mke wa mtu na pia ni mama.

Mitandaon, watu hawakuwa na tatizo na Huddah kujiita binti wa mtu na mfanyibiashara kwa sababu hilo linafahamika wazi kuwa ana ufanisi mkubwa sana katika bidhaa zake za kujipodoa.

Kivangaito kilikuwa pale alipojiita mke wa mtu na mama. Wengi walitaka kujua ni lini amepata mtoto kwa sababu kwa muda mrefu amekuwa akionekana kulipuulizia mbali kabisa suala la kupata mtoto – kwa wakati mmoja hata akimsuta mwanasosholaiti mwenzake Vera Sidika kwa kupata mtoto na kumpakia kila mara kwenye mitandao ya kijamii.

“Mimi ni mfanyibiashara mkubwa, binti, mama na mke wa mtu,” Huddah aliandika.

Baadae aliposutwa vikali, alirudi kwenye instastories zake na kupakia michambo mingine huku akijipiga kifua kuwa mtu jina lako ndilo utambulisho na biashara yako kwa hiyo hufai kukubali mtu kulichafua kwa njia hasi ukiangalia.

“Nihukumu kulingana na watu ambao ninawakwepa maishani mwangu. Jina lako ni chapa ya brand yako, usimkubalie mtu kulitumia vibaya,” Huddah alisema.

Hata hivyo, wengi wakionekana kupinga suala lake kuwa mke wa mtu na kuwa mama mtoto, baadhi walimtetea wakisema kuwa huenda aliolewa kinyemela na hata kuasili mtoto pasi na Wakenya kujua kwani kwa miaka ya hivi karibuni, Huddah hajakuwa akipakia maendeleo ya maisha yake mitandaoni zaidi ya biashara yake tu.