"Waliosema nina'date na Zuchu si kweli wanazusha!" Diamond amruka Zuchu

Wiki kadhaa zilizopita alikiri wazi kuwa ni mpenzi wake lakini safari hii ameibuka na jipya la kukanusha kauli ya awali.

Muhtasari

• Wawili hao kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa wamekuwa wakisemekana kuchumbiana na hivi karibuni wote walikiri kuwa wapenzi.

• Wengine wanahisi ni kiki wanafukuzia mitandaoni na wengine pia wakisema huenda ni wapenzi wa kweli.

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Sakata la Diamond Platnumz na msanii chini ya lebo yake ya WCB Wasafi, Zuchu linaendelea kuchukua mkondo changamano baada ya msanii huyo kujitokeza wazi na kukana kuchumbiana na Zuchu licha ya awali wawili hao kunyoosha maelezo kuwa ni wapenzi.

Diamond katika wimbo wake mpya wa Chitaki, kuna vesi moja ambayo anasikika akisema kuwa wanaosema anachumbiana na Zuchu ni wazushi tu wanaotafuta sababu ya kuendela kumsema yeye na msanii wake Zuchu.

Katika kipande hicho cha wimbo wake ambapo anaonekana kama anammruka na kumsaliti Zuchu kimapenzi, anambembeleza mpenzi wake mpya huku akimwambia kuwa maneno anayoyasikia kuwa anamvizia Zuchu si kweli hata kidogo.

“Wewe ndio mwisho wa reli, kwako naweka nukta. Waliokuambia natoka na Zuchu si kweli wanazusha. Wao ndio kazi yao sisi kutuhukumu…” Diamond anasikika akiimba.

Kipande hiki cha maneno kwenye wimbo wa Diamond kimezua mjadala mkali miongoni mwa wanamitandao ambao sasa wanahisi kama anamchezea shere Zuchu baada ya awali kukiri mapenzi yake kwake. Lakini pia kuna wengine ambao wanahisi ni utunzi tu wa kubuni katika wimbo wala maneno hayo hayana ukweli wowote kwani wawili hao ni mtu na mpenzi wake.

Ikumbukwe wiki kadhaa zilizopita wakakti wa uzinduzi wa albamu ya Jux – King of Hearts, Diamond aliyekuwa amealikwa pale alipanda jukwaani na kutamka wazi kuwa wimbo wake pendwa katika albamu hiyo ulikuwa ule Jux alimshirikisha Zuchu, huku akitamka kuwa ni “Wimbo Jux aliomshirikisha mke wangu Zuchu.”

Zuchu kwa upande wake pia hakuachwa nyuma kwani kkatika video moja ambayo alionekana akiulizwa maswali na rafiki yake, msichana huyo alimuonesha picha ya Diamond na kumuuliza kama anamjua na bila kusita Zuchu aliidakia na kusema kuwa, “Ndio huyo mpenzi wangu,”

Kwa muda mrefu, Diamond na Zuchu wamekuwa wakisemekana kuchumbiana nyuma ya pazia katika kile ambacho kilitajwa kuwa ni kujaribu kukwepa kamera kali na za siri kutoka kwa mapaparazi ambao wanawaandamana kila nukta na sekunde iendayo kwa Mungu.