Najua huwezi kumfikiria mwanamke mwingine kama unavyonifikiria mimi - Vishy amwambia Stevo

Vishy alisema yeye ndiye mwanamke wa pekee aliyemtendea Stevo Simple Boy haki ya kumpenda kabla aote pembe na kumtema.

Muhtasari

• Alimwambia kuwa hakuna mwanamke mwingine ataibuka maishani mwake kumpagawisha kama yeye.

• Hivi majuzi, Stevo alisema ana mwanamke ambaye wamechumbiana kwa miaka mingi na ambaye anatarajia kumuoa mwaka 2023.

Vishy amzomea Simple Boy
Vishy amzomea Simple Boy
Image: Instagram

Mwanablogu wa YouTube anayechipukia Pritty Vishy amemtumia aliyekuwa mpenzi wake Stevo Simple Boy ujumbe wa kimadharau huku akimtaka kukubali kuwa hatowahi kupata mwanamke mwingine kama yeye.

Kupitia kwenye Instastories zake, Vishy alimchamba Simple Boy akisema kuwa alikuwa anajifanya huko  hahisi kumkosa Vishy lakini nyuma ya pazia anatamani tu lile lililotokea mapema mwaka huu kupelekea kuachana kwao wala lisingetokea.

Vishy alimtaka msanii huyo wa Freshi Barida kukoma kujiliwaza na kauli kuwa hamfuatilii na badala yake kukubali kuwa yeye ndiye mwanamke wa pekee aliyemfanyia haki kipindi wanachumbiana.

“Atakuwa anajishaua na kujishebedua eti ‘simfuatilii sana’, kaka kubali mimi ndiye mwanamke wa pekee niliyekufanyia haki,” Pritty Vishy alimwambia Stevo.

Mwanadada huyo ambaye amegonga vichwa vya habari kwac wingi mwaka 2022 aliwachamba pia wale wote waliokuwa wakimsema kuwa ni yeye alikuwa anamfuatilia Stevo baada ya kuachana.

Aliwaambia kufunguka macho na sasa kugundua kuwa Stevo licha ya kujiita mume wa mtu bado anahisi wangerudiana naye, jambo ambalo alidokeza kuwa huenda halitokaa likatokea.

“Nyinyi wote mlikuwa mnanikandia eti, Pritty Vishy hajakubali kuachwa, sasa nafikiri nyinyi wote mmeona kuwa mume wa mwafulani hajakubali kuachwa,” Vishy alitamba kwa madaha na mikogo.

Pia alitumia fursa hiyo kutoa wosia kwa mwanadada ambaye anachumbiana kwa sasa na Stevo Simple Boy.

“Kwako wewe mwanadada unayechumbiana na Stevo Simple Boy, hatowahi kukufikiria vile ananifikiria. Katu huwezi kumshinda Pritty Vishy,” alisema na kumalizia kwa emoji za kucheka.