Sakata la baba halisi wa mtoto wa Hamisa Mobetto lazidi kuchafua hewa, Diamond azungumza

Mwanzoni wa Desemba, jamaa kwa jina Mpoki alipasua mbarika kuwa mtoto si wa Diamond bali ni wa Billnass.

Muhtasari

• Mpoki alichafua hewa aliposema kuwa ana ukweli mtoto wa Mobetto babake si Diamond.

• Sakata hilo limekuwa likizungumziwa kwa muda na safari hii Diamond aliamua kunyoosha maelezo kamili.

Sakata la mtoto wa Mobetto lazidi kuchafua hewa
Sakata la mtoto wa Mobetto lazidi kuchafua hewa
Image: Instagram

Kwa takribani mwezi mmoja sasa, sakata linalohusisha baba halali wa mtoto wa Hamisa Mobetto limekuwa likichukuwa mkondo tofauti.

Haya yalizuka wakati jamaa mmoja alifanya mahojiano ya moto kusema kuwa mtoto wa Hamisa Mobetto ambaye kwa muda mrefu amekuwa akijulikana kuwa ni wa aliyekuwa mpenzi wake Diamond Platnumz siye bali baba halali kulingana na jamaa huyo alikuwa ni mwanamuziki Billnass ambaye ni mume wa Nandy.

Hamisa Mobetto alijitokeza wazi wakati wa sakata hilo na kupinga vikali maneno hayo lakini wasanii Billnass na Diamond hawakuwahi kulizungumzia hata kidogo.

Juzi katika mahojiano ya kipekee na runinga ya Wasafi, Diamond kwa mara ya kwanza alizungumzia suala hilo na jibu lake lilikuwa fiche ambalo linahitaji uchanganuzi wa kina ili kubaini alichokuwa akimaanisha.

Diamond alisema kuwa hakuwa tayari kulizungumzia hilo kwa sababu linahusu mtoto mdogo ambaye hajajitambua na kuwataka wanaomuuliza iwapo yeye ni baba halali kulielekeza swali hilo kwa mama mtoto Hamisa.

Sitaki kumuhukumu mtoto Kwa sababu ni Malaika . Na muda mwingine Vitu kama hivi vinaweza kumkosesha Mtoto Haki zake za Kimsingi . Hizi Habari nimeanza kuzisikia Kitambo Sana Lakini Siku zote Mama ndiye anayejua Baba wa Mtoto,” Diamond alisema.

Kwa zaidi ya miaka miwili sasa, Diamond hajawahi kumtakia Dylan ambaye ni mtoto wake na Mobetto kheri ya siku njema ya kuzaliwa na wala kupakia picha yake wakati anasherehekea kuzaliwa, kama ambavyo huwa anafanya kwa watoto wake na Zari na Tanasha.

Wiki jana mamake, Mama Dangote alifanya kufuru ya mwaka alipomtangaza wazi mtoto wa Tanasha Donna, Naseeb Junior kuwa ndiye mrithi halisi wa Diamond katika biashara zake za Wasafi, tamko ambalo lilizua gumzo kali mitandaoni ambapo wengine walimtaka kuwatambua watoto wengine kama huyo wa Mobetto na wawili wa Zari Hassan.