Esma Platnumz afurahia mtoto wake kufuzu mtihani wa kitaifa wa kidato cha pili

Esma alifichua mwaka 2021 kuwa Tahiya, analipiwa kari na Diamond Platnumz.

Muhtasari

• Esma, ambaye anaendesha biashara ya mavazi, alisema anajitegemea na anaridhika hata bila kupata matunzo kutoka kwa wanaume ambao amezaa nao watoto wawili.

Esma amsherehekea mtoto wake aliyefaulu mtihani.
Esma amsherehekea mtoto wake aliyefaulu mtihani.
Image: Hisani

Mjasiriamali Esma Platnumz ambaye ni dada mkubwa wa mwanamuziki Diamond Platnumz ni mtu mwenye furaha baada ya mtoto wake kufuzu kwa divisheni ya kwanza katika mitihani ya kidato cha pili nchini Tanzania.

Mtoto huyo wa kwanza kwa jina Tahiya Platnumz alifaulu vizuri katika mitihani ya kitaifa ambayo ilitangazwa Alhamisi nchini humo na mamake, Esma hakuchelewa kuwataarifu wafuasi wake wengi kwenye ukurasa wake wa Instagram kuhusu mafanikio ya mwanawe.

Esma alimtaja binti wake kama mweledi wa masomo huku akimuombea mema katika safari inayoendelea ya masomo huku akimtaja kuwa alifuata akili za wazazi wake

Kama mzazi wako nakupa hongera sana Binti yangu umefuata akili ya Wazazi wako na imani kidato cha nne utatushangaza zaidi Inshallah Mungu atazidi kukusimamia najua hapo umenuna umekataa nisipost ila kama mzazi natamani dunia yote ione mtoto wangu ulivyojitahidi Mungu akulinde,” Esma aliandika.

Inaarifiwa kuwa mtoto huyo hakuwa amefurahishwa na matokeo hayo na alikuwa hataki mamake achapishe matokeo yake mitandaoni huku bibi yake, mamake na Diamond Mama Dangote akisema yeye alimwambia afute wala mtu asione.

Kwa upande wake, Uncle Shamte ambaye ni mpenzi wa mama Dangote alimhongera binti huyo na kusema kuwa akili za mzazi alizichukua kwa mikono yake miwili.

“Akili ya mama yake kachukua mikono miwili,” alisema Uncle Shamte.

Esma alifichua mwaka 2021 kuwa Tahiya, bintiye mkubwa, anatunzwa na Diamond Platnumz, ambaye hulipa karo na mahitaji ya shule.

Esma, ambaye anaendesha biashara ya mavazi, alisema anajitegemea na anaridhika hata bila kupata matunzo kutoka kwa wanaume ambao amezaa nao watoto wawili.