Harmonize kuacha kuimba nyimbo kwa lugha ya Kiswahili, "Bongo mimi ni namba 1"

Harmonize alisema wimbo wa mwisho atakaoutoa kwa lugha ya Kiswahili ni Ijuma hii.

Muhtasari

• Lugha ya Kiswahili imekuwa ikizua mjadala jinsi inazuia miziki ya Afrika Mashariki kutopenyeza kwenye masoko ya ughaibuni.

• Wasanii wengi akiwemo Harmonize wamekuwa wakijitahidi kutunga mashairi kwa lugha ya Kiingereza kama njia moja ya kupenyeza kimataifa.

Harmonize kutoa wimbo wa mwisho wa Kiswahili Ijumaa.
Harmonize kutoa wimbo wa mwisho wa Kiswahili Ijumaa.
Image: Instagram

Harmonize, mkurugenzi mtendaji katika lebo ya Konde Music Worldwide amedokeza kuwa hivi karibuni ataacha kufanya nyimbo kwa lugha ya Kiingereza.

Msanii huyo ambaye hajapoa kipindi chote cha Ramadani licha ya kuwa Muislamu kamili amedokeza kuwa Ijumaa hii ndio ataachilia wimbo wake wa mwisho ambao umetungwa kwa lugha ya Kiswahili.

“Ijumaa hii nitaachia wimbo wangu wa mwisho kwa lugha ya Kiswahili, angalau kwa mwaka huu,” Harmonzie alisema huku akidokeza kuwa maudhui ya wimbo huo yatakuwa ya walengwa wenye umri wa miaka Zaidi ya 18.

Itakumbukwa mapema wiki hii, Harmonize alidokeza kuwa yuko Zanzibar kwa ajili ya video, ambapo alifichua tayari amefanya video tano kwa mfululizo.

Baada ya kusutwa vikali kwa tamko lake kuwa ataacha kuimba Kiswahili licha ya nyimbo hizo maarufu Bongo Fleva kumtoa kwenye lindi la umaskini, Msanii huyo wa kujitapa alisema kuwa bado yeye ndiye mfalme wa Bongo Fleva na bila yeye hakuna miziki hiyo ya Kiswahili.

“Konde Boy ni Bongo Fleva. Bongo Fleva ni Kondeboy. Niite namba moja, hakuna amewahi kunifikia ustadi wangu katika kutuna mashairi ya Kiswahili. Mimi ni wa moto na ni muda wangu, nyinyi jua hivyo. Sapoti yenu na mapenzi yenu yamesababisha hili litokee, tukutane Ijumaa. Kabla uongee pumba kwanza jua unaongea kuhusu msanii ambaye ameteuliwa mara nyingi Zaidi kuwania tuzo za TMA,” Harmonize alisema.

Msanii huyo amekuwa akijitahidi katika kutunga mashairi kwa lugha ya Kiingereza, baadhi ya mashabiki wake wakihisi kwamba ameimarika pakubwa katika mashairi yake kwa lugha hiyo ya Kigeni.

Kwa muda mrefu kumekuwa na dhana kwamba lugha ya Kiswahili ndio inayofanya miziki ya Afrika Mashariki haipenyi kwenye masoko ya miziki ya ughaibuni kulinganishwa na miziki ya kutoka Afrika Kusini na Magharibi mwa Afrika.

Otile Brown mwaka jana baada ya kurejea nchini kutoka kwa ziara yake ya kimuziki Marekani, alisema kwamba alijifunza kitu kimoja kuwa Kiswahili kinakwaza sana maendeleo ya wasanii wa Afrika Mashariki kimuziki na hivyo kusema kuwa alikuwa na wazo la kujaribu kutunga mashairi Zaidi kwa lugha ya Kiingereza ili kuwafikia mashabiki wengi kote duniani.