Pastor T amuomboleza Videographer wa Mr Seed aliyefariki katika ajali

Mr Seed na timu yake walikuwa wanaelekea Naromoru wakati gari lao lilipata ajali ambapo alinusurika kwa jeraha la nyonga.

Muhtasari

• "Ulikuwa kito chenye karama katika Ufalme wa Mungu tangu siku za nyimbo za hali ya juu. Pumzika na Malaika,” Pasta T Mwangi aliomboleza.

Ambroze Mburu Khan, videographer wa Mr Seed.
Ambroze Mburu Khan, videographer wa Mr Seed.
Image: FACEBOOK

Wikendi iliyopita, msanii wa injili Mr Seed na wenzake walihusika katika ajali mbaya ya barabarani ambayo iligharimu maisha ya baadhi ya waliokuwemo na msanii huyo.

Katika msururu wa taarifa zilizochapishwa na mke wake Nimo Gachuiri, Mr Seed alinusurika ajali hiyo japo kwa majeraha mabaya ambapo madaktari walimtaka kutojihusisha na shughuli yoyote kwa muda wa wiki mbili zijazo.

Baadae ilibainika kwamba miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mpiga picha wa muda mrefu wa Mr Seed, Ambroze Mburu Khan.

Mchungaji T Mwangi amekuwa mtu wa hivi karibuni kumuomboleza kijana huyo ambaye muda mwingi alikuwa nyuma ya kamera na hakuwa anajulikana na wengi licha ya kuzalisha kazi za wasanii wa injili ambazo zimekuwa zikifanya vizuri.

Pasta T alisema kuwa tasnia ya muziki wa injili imepoteza pakubwa huku akimkumbuka Khan kutoka enzi za awali kabisa ambapo wamekuwa wakifanya kazi pamoja.

“Pumzika kwa amani kaka. Ulikuwa kito chenye karama katika Ufalme wa Mungu tangu siku za nyimbo za hali ya juu. Pumzika na Malaika,” Pasta T Mwangi alisema.

Akiongea baada ya ajali hiyo, Nimo alifichua kuwa yeye na mumewe Mr Seed walikuwa wakiendesha gari kuelekea Naromoru kwa magari tofauti na marafiki zao wakati lile gari ambalo Seed alikuwa anasafiria nao lilipopata ajali.

Mama wa mtoto mmoja alishiriki picha inayoonyesha majeraha madogo ya Seed mikononi mwake na kusema:

"Siamini mume wangu yu hai. Sijawahi kuwa na hofu kama hii maishani mwangu." Kushiriki mabaki ya gari."

Nimo alifichua kuwa baadhi ya marafiki zao walipoteza maisha na baadae ilikuja kubainik kuwa Khan, ambaye ni mpiga picha wa Seed ni miongoni mwa wale waliofariki katika ajali hiyo.

Ajali hiyo ilimuacha Mr Seed akiwa na jeraha la nyonga.