Mustafa: Hiki ndicho nitafanya kuhakikisha sirudi kwenye mkwamo wa kifhedha tena

Msanii huyo alisema alifanya mjengo kwa mwaka mmoja akificha tattoo kwa sweta kubwa na uso kwa kuvalia barakoa.

Muhtasari

• Mustafa alielezea kwa ufasaha kwamba atakuwa anatenganisha akaunti mbili, moja yake na nyingine ya mamake.

Msanii mkongwe kutoka Ogopa Djs, Coonel Mustafa
Msanii mkongwe kutoka Ogopa Djs, Coonel Mustafa
Image: Colonel Mustafa (Instagram)

Rapa mkongwe Colonel Mustafa kwa mara ya kwanza amevunja kimya chake baada ya marafiki na wasamaria mwema kujitokeza pakubwa ili kumkwamua kifedha.

Sakata la msanii huyo lilipata upwanyunyu kwenye mwanga wa mitandao ya kijamii baada ya video kuenezwa ikimuonesha akifanya kazi ngumu kwenye mradi wa ujenzi.

Katika mkutano na wanahabari wa mitandaoni, Mustafa alifunguka kwamba amekuwa akifanya kazi hiyo kwa Zaidi ya mwaka mmoja pasi na mtu yeyote kumgundua kwani alikuwa anavalia sweta kubwa la kuzifunika tattoo zake mikononi lakini pia kuficha uso kwa kuvalia barakoa mda wote.

“Nilifanya kwa siri sana Zaidi ya mwaka mmoja, nilijaribu sana kutojulikana kwa kuvaa sweta kuficha tattoo pamoja pia na barakoa. Nilijaribu sana,” Mustafa alisema huku machozi yakimlengalenga.

Msanii mwenzake ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Starehe Charles Njagua Kanyi almaarufu Jaguar alifichua kuwa tayari wameshachangisha karibia shilingi milioni moja za Kenya na wiki kesho majaaliwa watamtembelea mama yake ambaye anaugua saratani ili kumppa salamu za pole kwa ugonjwa na kumkabidhi mzigo huo.

Alipoulizwa jinsi gani atajipanga ili asije kujirudi kwenye mkwamo wa kifedha siku za mbeleni tena, Mustafa alielezea kwa ufasaha kwamba atakuwa anatenganisha akaunti mbili, moja yake na nyingine ya mamake ili kuhakikisha kwamba anapoendelea kujukumikia matibabu ya mama, pia kwa upande mwingine mambo yake hayakwami.

“Kitu cha kwanza ni kutenga akaunti mbili ya mama na yangu, pesa yoyote nitakuwa ninapata nitatenga kiasi kwa akaunti yake na nyinginge kwa akaunti yangu,” Mustafa alisema.

Pia alisema pesa hizo ambazo atasaidiwa atahakikisha ameboresha maisha ya mama yake kwa kumalizia ujenzi ambao ulikuwa umekwama baada ya saratani kumsakama.

“Baada ya mama kupana afueni kutokana na saratani, nitammalizia ujenzi wa kibanda chake ambao ulisimama kwa muda. Kuna nyumba ambayo anaishi na haiku vizuri. Nitamsaidia juu chini kumfurahisha venye anataka,” Mustafa alisema kwa sauti ya shukurani.

Msanii huyo alifichua kuwa mamake ni Muislamu na kwa muda amekuwa akitamani siku moja kwenda kuhiji Mecca, mji unaotajwa kuwa mtakatifu Zaidi kwa dini ya Kiislamu huko Saudi Arabia.

“Amekuwa akisema sana anatamani kwenda kuhiji Mecca, siku moja nitampeleka na hiyo itakuwa ni kutimiza ndoto yake na atazidi kuniombea.”