Okanga amemkashifu Kanyari kuwazomea watu wanaoenda kanisani bila sukari, majani

Okanga alimshtumu vikali Kanyari haswa kutokana na video ya hivi majuzi ambayo iliibuliwa ikimuonesha pasta Kanyari akihubiri katika kanisa lake kuhusu waumini wanaomwendea mikono mitupu.

Muhtasari

• Pia aliweza kuzungumzia suala la kifo cha utata cha dadake Kanyari ambaye anashukiwa kuuawa na mwanamume katika nyumba ya AirBnB mtaani South B.

OKANGA NA KANYARI
OKANGA NA KANYARI
Image: Maktaba

Mtetesi mkali wa sera za kinara wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, Nuru Okanga amejitokeza kwa mara nyingine tena baada ya kimya cha muda, na safari hii aeelekeza mtutu wa bunduki ya mashambulizi yake kwa mchungaji Victor Kanyari.

Kupitia kwa klipu fupi ambayo imeenezwa kwenye jukwaa la X, Okanga alimshtumu vikali Kanyari haswa kutokana na video ya hivi majuzi ambayo iliibuliwa ikimuonesha pasta Kanyari akihubiri katika kanisa lake kuhusu waumini wanaomwendea mikono mitupu.

Okanga alimtaja Kanyari kama mmoja wa matapeli katika kanisa na kusema kwamba anafaa kuaibika kwa kuwashrutisha waumini wake kumbebea vitu vikiwemo sukari na majani wakati wanaenda kumuona – kama kweli wanamchukulia kama baba wao wa kiroho.

“Kanyari ni mkora… sasa leo watu wa Kanyari watanipigia simu kunitisha, Kanyari ni mkora. Na narudia kusema Kanyari ni mkora na ni tapeli. Alisema juzi eti usipoenda kwa kanisa na sukari anakufukuza, wewe ji jambazi na mwizi,” Okanga alisema kwa ujasiri.

Pia aliweza kuzungumzia suala la kifo cha utata cha dadake Kanyari ambaye anashukiwa kuuawa na mwanamume katika nyumba ya AirBnB mtaani South B.

Okanga alisema kwamba Kanyari hafai kuwa mtu anahubiria watu waokoke wakati dadake ambaye ni marehemu sasa alikuwa anajihusisha kimapenzi na mwanamume tapeli wa mapenzi.

Itakumbukwa siku chache zilizopita tuliripoti kuhusu video ambayo haijulikani ni ya lini ikimuonyesha Kanyari akiwapa onyo waumini katika kanisa lake kuhusu kuenda kumuona wakiwa mikono mitupu.

Kanyari katika video hiyo alionekana akisema kwamba hatoruhusu muumini yeyote kwenda kanisani mikono mitupu, akiapa kuwafukuza endapo wataendelea kwenda mikono mitupu.

Mchungaji huyo mwenye misimamo mikali ya utata pia alisema kwamba hatokubali wanaompelekea pesa kati ya shilingi mia mbili na mia tano.