Msanii Jaguar awasilisha mchango wa rais Ruto kwa msanii mgonjwa Peter Miracle Baby

"Na kutoka leo hatutawahi changa tena. Pesa yote ya matibabu ya Peter itasimamiwa na mheshimiwa rais William Samoei Ruto,” Karangu Muranya alisema.

Muhtasari

• Hatua hii inajiri siku chache baada ya mwanaharakati Eric Omondi kupitia kwa wakfu wake wa Sisi Kwa Sisi kuchangisha pesa na kumtoa Miracle Baby Hospitalini.

Miracle Baby
Miracle Baby
Image: Instagram

Ni afueni kwa msanii wa gengetone na Mugithi, Peter Miracle Baby baada ya rais Ruto kudaiwa kutoa mchango wake kwake kwa ajili ya matibabu yake.

Katika video ambayo imekuwa ikienezwa mitandaoni, msanii na mwanasiasa Charles Njagua Kanyi maarufu kama Jaguar aliwasilisha shilingi laki tatu taslimu na kusema kwamba ni mchango wa rais kwa msanii huyo.

Msanii Peter Miracle Baby amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa tangu mwezi Januari mwaka huu ambapo mpenzi wake Carol Katrue alisema alifanyiwa upasuaji mara tatu kutokana na hitilafu kwenye matumbo yake.

Katika video hiyo, Jaguar pamoja na mhisani Karangu Muraya walionesha burunguti hilo la laki 3 taslimu na kusema kwamba ni mchango kutoka kwa rais, huku wakielekeza kwamba msanii huyo apelekwe hospitali.

“Kwa hiyo hii ni shilingi 300k kutoka kwa rais [Ruto] ambayo ametumana hapa kwa kina Peter [Miracle Baby] na ameahidi kuwa Peter apelekwe hospitali. Na kutoka leo hatutawahi changa tena. Pesa yote ya matibabu ya Peter itasimamiwa na mheshimiwa rais William Samoei Ruto,” Karangu Muranya alisema huku akimkabidhi Jaguar bunda hilo ili kuwapokeza wanafamilia wa Miracle Baby.

Hatua hii inajiri siku chache baada ya mwanaharakati Eric Omondi kupitia kwa wakfu wake wa Sisi Kwa Sisi kuchangisha pesa na kumtoa Miracle Baby Hospitalini.

Kwa mujibu wa Omondi, Miracle Baby alikuwa amekwamba hospitalini baada ya kukaa hap tangu Januari 17 ambapo kwa wakati mmoja alifanyiwa upasuaji mara tatu ndani ya kipindi kifupi.