Octopizzo aeleza kwa nini amekuwa akitoa ngoma 3 pekee kwa kila mwaka

“Hata ukiangalia, tangu sisi tuanze, kwa mfano mimi nilitambulika kimuziki 2012 lakini mpaka sasa hivi bado tuko kwa game, si eti kwa sababu tunapenda bali ni juu hakuna wasanii wapya." alisema.

Muhtasari

• Katika tuzo za EAEA 2024, Octopizzo alishinda tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa wimbo wake wa ‘Wapi Compe’.

 

Msanii wa kuchana mistari ya muziki Octopizzo
Msanii wa kuchana mistari ya muziki Octopizzo
Image: Instagram//Octopizzo

Msanii wa muziki wa Rap, Octopizzo ameibuka na sababu ya kueleza kwaa nini siku hizi hana haraka ya kuachia ngoma nyingi.

Octopizzo ambaye alikuwa anazungumza kwenye hafla ya kutolewa kwa tuzo za EAEA 2024 jijini Nairobi usiku wa Jumapili, alisema kwamba miaka ya hivi karibuni, amekuwa akiachia ngoma 3 pekee kila mwaka, akisema hana shinikizo tena.

Msanii huyo alisema kwamba Kenya hakuna wasanii wapya wanaowapa changamoto wasanii walioanza muziki kitambo na hivyo kila mwaka unawapata wasanii ni wale wale kutoka miaka 10 iliyopita.

Rapa huyo wa kutoka Kibera alisema kwamba Kenya kuna wasanii Zaidi ya elfu 15 lakini ukihesabu wasanii wanaofanya muziki kama biashara hawawezi kuzidi 10.

“Kenya tuko na sekta ya muziki lakini hatuna biashara ya muziki. Wasanii wanafanya biashara kwa ngoma hawawezi fika hata 10, lakani ukiangalia kwa MCSK wasanii wamejisajili ni Zaidi ya 16,000,” Octopizzo alisema.

“Hata ukiangalia, tangu sisi tuanze, kwa mfano mimi nilitambulika kimuziki 2012 lakini mpaka sasa hivi bado tuko kwa game, si eti kwa sababu tunapenda bali ni juu hakuna wasanii wapya. Mimi natoa ngoma 3 kwa mwaka siku hizi juu sina mbio. Nilishatengeneza kitu nilikuwa nataka kutengeneza, sasa hivi nafanya ngoma juu napenda ngoma, yaani nikikaa bila kutoa ngoma inanibore,” aliongeza.

Katika tuzo za EAEA 2024, Octopizzo alishinda tuzo ya wimbo bora wa Hip Hop katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa wimbo wake wa ‘Wapi Compe’.