Rosie, watoto wake waonekana kupendeza wakianza likizo ya siku 3 Maasai Mara

Wanne hao walionekana kuwa na furaha sana na shauku kubwa ya safari iliyokuwa mbele yao.

Muhtasari

•Expeditions Maasai Safaris ilithibitisha kuwa Rozah pamoja na watoto wake watatu walikuwa safarini kuelekea hifadhi hiyo.

•Tabasamu nzuri sana zilionekana kwenye nyuso zao.

na watoto wake watatu kabla ya kupelekwa Maasai Mara mnamo Desemba 14, 2023.
Rozah Rozalinah na watoto wake watatu kabla ya kupelekwa Maasai Mara mnamo Desemba 14, 2023.
Image: EXPEDITIONS MAASAI SAFARIS

Mwanadada wa Kenya ambaye alivuma sana kwa siku kadhaa mapema mwezi huu, Roseline Atieno almaarufu Rozah Rozalina ameanza rasmi ziara yake ya siku tatu katika Hifadhi ya Kitaifa ya Maasai Mara kwa hisani ya Expeditions Maasai Safaris.

Siku ya Alhamisi, kampuni hiyo maarufu ya utalii inayoongozwa na mtaalamu wa masuala ya utalii Pancras Karema ilithibitisha kuwa Rozah pamoja na watoto wake watatu walikuwa safarini kuelekea hifadhi hiyo.

Expeditions, katika taarifa yake ilihakikisha kwamba mwanadada huyo ambaye amekuwa akifanya kazi ya ulezi nchini Lebanon pamoja na familia yake watakuwa na kipindi kizuri katika hifadhi hiyo ya kitaifa.

"Tulimwahidi Rozah na familia yake safari ya kukumbukwa ya siku 3, tunatimiza ahadi hiyo.. Maasai Mara tunaja," taarifa ya Expeditions Maasai Safaris ilisoma.

Waliambatanisha taarifa hiyo na picha nzuri za Rosie akiwa na familia yake ndogo walipokuwa wakisubiri kupelekwa Maasai Mara kwa gari la kampuni hiyo.

Katika picha hizo, Rozah pamoja na watoto wake wote watatu walionekana kuwa na furaha sana na shauku kubwa ya safari iliyokuwa mbele yao.Tabasamu nzuri sana zilionekana kwenye nyuso zao.

Kampuni ya Expeditions Maasai Safaris ilimpa mwanadada huyo anayetoka kaunti ya Siaya na watoto wake safari isiyo na malipo ya siku tatu katika hifadhi kubwa ya kitaifa ya Maasai Mara baada ya kugusa mioyo ya watu wengi kupitia video ya kihisia yeye akiiga familia ya Lebanon ambayo amekuwa akifanyia kazi iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii. Katika video hiyo, watoto ambao amekuwa akiwatunza katika miaka miwili iliyopita walionekana kupata ugumu kumuaga, ishara kuwa walimpenda..

Kufuatia kujitolea ambako Rosie aliionyesha kwa kazi yake nchini Lebanon, Expeditions Maasai Safaris mapema wiki jana ilimsherehekea kwa kumpa likizo ya bure katika mbuga kubwa la Masai Mara ili kusherehekea na familia yake.

"Tuliguswa moyo sana na hadithi ya Rozah na uhusiano wake wa ajabu na familia anayoitumikia Lebanon. Kujitolea na upendo wake unajumuisha roho ya huruma tunayothamini katika Safari za Safari za Maasai," alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Expeditions Maasai Safaris, Bw Pancras Karema wakati akimtunza Rosie mapema wiki jana .

Rosie na familia yake walipewa likizo hiyo ili waweze kuzama katika turathi tajiri za kitamaduni za Kenya, wanyamapori wa aina mbalimbali na mandhari nzuri, na kuhakikisha kipindi kizuri kisichosahaulika.