Safiri salama:Baba yake waziri wa ardhi Karoney azikwa nyumbani kwake

Muhtasari

•Mzee Karoney alifariki baada ya kugongwa na pikipiki

•Amezikwa nyumbani kwake kufuatia kanuni za kiislamu

•Karoney alikuwa na miaka 74, ni baba yake waziri wa ardhi Faridah Karoney

Mzee Edward Kiprotich Karoney, babake waziri wa Ardhi Farida Karoney, amezikwa nyumbani kwake Kapsabet siku moja tu baada ya kufariki kwenye ajali ya barabara.

Mzee huyo alizikwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za dini ya Kiislamu baada ya kupoteza maisha yake Jumanne alipogongwa na bodaboda.

Kulingana na ripoti, alikuwa ameegesha gari lake na mara tu alipokuwa akivuka barabara upande wa pili aligongwa na pikipiki na kuripotiwa kufariki alipofikishwa katika hospitali ya Kapsabet.

Mawaziri Prof George Magoha wa Elimu, Charles Keter wa Kawi, Waziri wa Utumishi wa Umma Margaret Kobia, Betty Maina wa Biashara, na mwenzao wa Maji Simon Chelugui walihudhuria mazishi hayo. Wakati wa hafla hiyo, mzee huyo alikumbukwa kama bingwa katika kupigania haki za mtoto wa kike.

Rais Uhuru Kenyatta aliwaongoza viongozi kumuomboleza mzee huyo kwa kutuma risala za rambirambi.

“Ni masikitiko tumempoteza Mzee Karoney wakati tunahitaji ushauri wake wa busara kama mzee. Tumepoteza mtu ambaye alithamini na alikuwa bingwa hodari wa elimu katika jamii yake kama inavyoonekana kupitia watoto wake." Aliandika Rais.

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi.

(Mhariri Davis Ojiambo)