MASHINDANO YA MAGARI KENYA

Fahamu barabara ambazo zitafungwa wakati wa mashindano ya magari

Waziri Matiang'i alitangaza kuwa sababu ya kufungwa kwa barabara hizo ni ili kuhakikisha usalama wakati wa mbio hizo.

Muhtasari

•Kupitia gazeti la serikali lililotolewa siku ya Jumanne, Matiang'i alitaja barabara tano kuu ambazo zitafungwa kwa magari yote ya kibiashara ambayo yana uzani wa zaidi ya tani 3 kati ya Alhamisi na Jumapili.

•Wenye magari mazito wameagizwa kuyaegesha kwenye kituo kitakachokuwa karibu itimiapo wakati wa kufunga barabara hizo na kusubiri hadi zifunguliwe.

Mashindano ya Safari Rally yakizinduliwa rasmi
Mashindano ya Safari Rally yakizinduliwa rasmi
Image: Hisani

Waziri wa maswala ya ndani, Fred Matiang'i ametangaza kuwa usafiri barabarani utaathirika kwa kipindi cha siku nje kufuatia mashindano mbio za magari yatakayoanza leo ( Juni 24).

Kupitia gazeti la serikali lililotolewa siku ya Jumanne, Matiang'i alitaja barabara tano kuu ambazo zitafungwa kwa magari yote ya kibiashara ambayo yana uzani wa zaidi ya tani 3 kati ya Alhamisi na Jumapili.

Alisema kuwa sababu ya kufungwa kwa barabara hizo ni ili kuhakikisha usalama wakati wa mbio hizo.

Barabara kuu ya kutoka Eldoret kuelekea Nakuru itafungwa siku ya Alhamisi, Juni 24, kuanzia mida ya saa sita usiku wa manane hadi saa moja usiku. Kituo cha kufungwa kitakuwa Eldoret.

Barabara kuu ya kutoka Kericho kuelekea Nakuru itafungiwa Kericho siku ya Ijumaa, Juni 24, kuanzia mida ya saa sita usiku hadi saa moja usiku.

Barabara kuu ya kutoka Nyahururu hadi Nakuru itafungiwa Nyahururu siku ya Jumamosi kuanzia saa sita usiku, mchana kutwa hadi saa moja usiku.

Barabara ya kuu ya Mombasa-Nairobi-Mai Mahiu hadi Naivasha itafungiwa Mlolongo siku ya Jumapili, Juni 27, kuanzia saa sita usiku wa manane hadi saa moja usiku.

Barabara ya kutoka Narok kuelekea Mai Mahiu itafungwa katika kituo cha Suswa kwa wakati huo.

Wenye magari mazito wameagizwa kuyaegesha kwenye kituo kitakachokuwa karibu itimiapo wakati wa kufunga barabara hizo na kusubiri hadi zifunguliwe.

Barabara ya kutoka Kikopey kuelekea Elementaita itabaki imefungwa kwa magari yote kuanzia Ijumaa, Juni 25 hadi Jumapili, Juni 27.

Maafisa wa polisi zaidi ya 1000 wamepelekwa Naivasha kwa ajili ya usalama kwenye hafla hiyo.

Mashindano haya ambayo yamesubiriwa kwa hamu na ghamu yatakuwa ya kwanza kufanyika nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 19 iliyopita.