Raila Jr alalamikia ORPP kwa kumsajili kama mwanachama wa ANC; Awapa siku moja kumsajili ODM

. Otiende amesema kuwa Raila Jr alipatwa na mshangao baada ya kugundua kuwa amenakiliwa kama mfuasi wa Mudavadi.

Muhtasari

•Kupitia wakili wake, Otiende Amollo, Raila Jr ameandikia ofisi hiyo barua ya malalamishi na kutaka mabadiliko kufanywa kabla  ya masaa 24 kuanzia jioni ya Jumatano

•Wakili Otiende Amollo  amedai kuwa maelezo ni ya uongo na yanaweza kusababisha madhara  kwa Raila Jr ambaye anajitambulisha na chama cha ODM. 

Raila Odinga Jr
Raila Odinga Jr
Image: Hisani

Raila Odinga Jr amelalamikia hatua ya ofisi ya  msajili wa vyama vya kisiasa(ORPP)  kumsajili kama mwanachama wa  chama cha ANC kinachoongozwa na Musalia Mudavadi bila idhini yake.

Mwanawe kinara wa ODM ameagiza ORPP kufutilia mbali usajili wake kama mwanachama wa ANC na kumsajili kama mwanachama wa ODM.

Kupitia wakili wake, Otiende Amollo, Raila Jr ameandikia ofisi hiyo barua ya malalamishi na kutaka mabadiliko kufanywa kabla  ya masaa 24 kuanzia jioni ya Jumatano. Otiende amesema kuwa Raila Jr alipatwa na mshangao baada ya kugundua kuwa amenakiliwa kama mfuasi wa Mudavadi.

Wakili huyo  amedai kuwa maelezo ni ya uongo na yanaweza kusababisha madhara  kwa Raila Jr ambaye anajitambulisha na chama cha ODM. 

"Mteja wetu analalamikia ukiukaji wa faragha  na kutumika kwa data yake ya kibinafsi kwa madai ya uongo bila idhini . Ametuhumiwa kuwa mwanachama wa ANC ilhali hajajiwasilisha ama kuidhinisha usajili huo na hana uhusiano wowote na chama cha ANC. Maelezo yenu ya uongo yanakiuka haki zake za kisiasa" Otiende aliandika.

Kwenye barua hiyo, Otiende amekumbusha ORPP kuwa iko na jukumu la kuthibitisha orodha ya wanachama wa  chama chochote cha kisiasa kabla ya kuitangaza. Alisema kuwa sheria inalinda data za faragha za Mkenya yeyote ili kuzuia kusajiliwa kwa mtu kwa chama fulani bila idhini.

"Tunaagiza ofisi yenu kufanya mabadiliko kwenye rekodi zenu haswa kufuta maelezo ya mteja kwa orodha ya wanachama wa ANC na kumuorodhesha vyema kama mwanachama wa ODM mara moja ndani ya kipindi cha masaa ishirini na manne yajayo toka mpokee barua hii. Baada ya kufanya hilo mtuandikie kuthibitisha" Aliandika Otiende.

Otiende aliagiza ofisi hiyo kufanya marekebisho kwenye rekodi za Wakenya wote kufuatia malalamiko yaliyotangazwa na Wakenya wengi mitandaoni.