Marafiki walichanga dhamana ya milioni 12 ndani ya masaa 3- Gachagua azungumza baada ya kuachiliwa

Alisema kuwa kesi ya ufisadi ambayo amekabiliwa nayo ni ya kizushi tu na imetengezwa na DCI kwa amri toka ikulu na kuwa alikuwa akisulubishwa kwa kuwa na msimamo kinzani wa kisiasa.

Muhtasari

•Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, mwandani huyo wa naibu rais William Ruto aliwashukuru wote walioshirikiana naye na kumuunga mkono kwa namna yoyote ile kwa kipindi cha siku tatu alizokuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri.

•Mawakili waliomwakilisha mbunge huyo ni pamoja na Kioko Kilukumi, Alice Wahome, Gladys Boss Sholei, Kipchumba Murkomen, Sylvanus Osoro, Irungu Kangata, Gibson Kimani, Paul Gacheru, Amos Kisiwi na Wycliffe Nyabuto.

Image: FACEBOOK//RIGATHI GACHAGUA

Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua ni mwenye bashasha baada ya kuungana tena na familia yake kufuatia kuachiliwa huru kwake siku ya Jumatatu.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Facebook, mwandani huyo wa naibu rais William Ruto aliwashukuru wote walioshirikiana naye na kumuunga mkono kwa namna yoyote ile kwa kipindi cha siku tatu alizokuwa amezuiliwa katika kituo cha polisi cha Gigiri.

Gachagua ambaye aliwachiliwa huru baada ya kulipa dhamana ya milioni kumi na mbili amefichua kuwa  marafiki wake ambao hakuwataja walimsaidia kuchanga kiwango hicho kikubwa cha pesa ndani ya masaa matatu tu.

"Nashukuru marafiki ambao walinisaidia kuchanga dhamana hiyo kubwa kwa rekodi ya  masaa matatu tu" Gachagua alisema.

Alisema kuwa kesi ya ufisadi ambayo amekabiliwa nayo ni ya  kizushi tu na imetengezwa na DCI kwa amri toka ikulu na kuwa alikuwa akisulubishwa kwa kuwa na msimamo kinzani wa kisiasa.

Hata hivyo aliwashukuru mawakili wake 10 kwa kumwakilisha kwenye kesi hiyo mbele ya hakimu mkuu Lawrence Mugambi.

"Nashukuru jamii ya 'hustler'  kwa ushirikiano. Nashukuru timu yangu ya mawakili 10  wakiongozwa na  Kioko Kilukumi. Nawashukuru pia maafisa wa polisi katika makao makuu ya DCI na kituo cha polisi cha Gigiri kwa kunionyesha heshima na utaalam wao katika kutekeleza majukumu yao" Gachagua alisema.

Mawakili 10 waliomwakilisha mbunge huyo ni pamoja na Kioko Kilukumi, Alice Wahome, Gladys Boss Sholei, Kipchumba Murkomen, Sylvanus Osoro, Irungu Kangata, Gibson Kimani, Paul Gacheru, Amos Kisiwi na Wycliffe Nyabuto.

Gachagua pia alishukuru familia yake kwa kusimama naye na watu wa Mathira na wengine  kwa kulalamikia kukamatwa kwake.

"Nashukuru mke wangu na vijana wangu kwa kusimama nami na kulinda boma letu wakati sikuwa. Na pia nashukuru watu wa Mathira, Kiambaa na ELdoret kwa kuashiria ghadhabu yao kwa namna moja au nyingine kufuatia matumizi ya mashirika ya kupambana na uhalifu kutesa  walio na msimamo tofauti wa kisiasa," Alisema Gachagua.

Hata hivyo alisema kuwa alifurahia kuona haki ikitendeka katika mahakama.