(+Picha) 'Ni siku ya kujivunia!' Mbunge Jicho Pevu asherehekea baada ya kuhitimu na shahada ya Uzamili

Wabunge wenzake na wandani wake wa mrengo wa Tangatanga, Ocar Sudi na Didmus Barasa ni baadhi ya walioandika jumbe zao za pongezi.

Muhtasari

•Mtangazaji huyo wa zamani alihitimu na shahada ya uzamili katika masuala ya kidiplomasia na sera za kigeni siku ya Ijumaa.

•Wanamitandao wengi ikiwemo wanasiasa mashuhuri walijumuika kumpongeza mbunge huyo wa muhula wa kwanza.

Image: TWITTER// MOHAMMED ALI

Mbunge wa Nyali Mohammed Ali almaarufu kama Jicho Pevu ni mtu mwenye raha sasa baada ya kuhitimu kutoka chuo kikuu cha Moi.

Mtangazaji huyo wa zamani alihitimu na shahada ya uzamili katika masuala ya kidiplomasia na sera za kigeni siku ya Ijumaa.

Jicho Pevu alitangaza fanikio hilo kupitia kurasa zake za  mitandao ya kijamii.

"Ni siku ya furaha aje! Nimewezana. Shahada ya uzamili katika masuala ya kidiplomasia na sera za kigeni kutoka chuo kikuu cha Moi, Eldoret. ALLAHU AKBAR" Ali alisema.

Wanamitandao wengi ikiwemo wanasiasa mashuhuri walijumuika kumpongeza mbunge huyo wa muhula wa kwanza.

Wabunge wenzake na wandani wake wa mrengo wa Tangatanga, Ocar Sudi na Didmus Barasa ni baadhi ya walioandika jumbe zao za pongezi.

"Hongera rafiki yangu na mwenzangu Mohammed Ali kwa kuhitimu. Bidii yako imelipa hatimaye. Nakutakia kila kitu kizuri. Endelea kung'aa" Sudi alimwandikia Ali.

"Hongera Jicho Pevu kwa kuhitimu. Uliwashinda Raila Odinga na Hassan Joho na kutwa kiti cha ubunge cha Nyali, sasa unatoboa dunia ya elimu kwa kuvunja rekodi yako mwenyewe" Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alimwandikia.

Hata hivyo, shabiki mmoja aliyetaka kujua wakati wanasiasa hupata nafasi ya kuketi chini na  kusoma alijipata pabaya baada ya kupokea jibu la kikejeli na kustaajabisha kutoka kwa mwanasiasa huyo.

"Hawa watu husoma saa ngapi?" Jamaa anayejitambulisha kwa jina @_dasiago mtandaoni wa Twiter aliuliza.

"Saa zile una kula muguka" Ali alimjibu.