Hofu baada ya jamaa kuua mpenzi wake mwanafunzi wa KMTC kisha kujisalimisha kwa polisi Loitoktok

Muhtasari

•Miriam Chepchirchir 22, ambaye alikuwa katika mwaka wake wa kwanza wa masomo ya chuo kikuu anadaiwa kuuawa na mpenzi wake Samson Kipkorir 27 asubuhi ya Jumamosi katika eneo la Kamukunji kufuatia mzozo wa mapenzi.

•Kisu ambacho kilitumika kutekeleza mauaji yale kilipatikana kwa nyumba ile ya marehemu ambayo ilijaa ushahidi kwamba kulikuwa na vita kubwa kabla ya mshukiwa kumwangamiza marehemu.

Marehemu Miriam Chepchirchir
Marehemu Miriam Chepchirchir
Image: HISANI

Mwanafunzi mmoja wa kike katika chuo cha KMTC tawi la Loitoktok anaripotiwa kufariki baada ya kudungwa kwa kisu na mpenzi wake.

Miriam Chepchirchir 22, ambaye alikuwa katika mwaka wake wa kwanza wa masomo ya chuo kikuu anadaiwa kuuawa na mpenzi wake Samson Kipkorir 27 asubuhi ya Jumamosi katika eneo la Kamukunji kufuatia mzozo wa mapenzi.

Inadaiwa  kwamba mshukiwa ambaye anafanya kazi maeneo ya Ruaraka alikuwa amemtembelea mpenzi wake usiku wa Ijumaa.

Baada ya kutekeleza mauaji yale mshukiwa anaripotiwa kujisalimisha mwenyewe katika kituo cha polisi cha Loitoktok kisha kuelekeza maafisa hadi kwa eneo la tukio.

Polisi walipofika kwa eneo la mauaji ili kuthibitisha madai ya mshukiwa walipata mwili wa Miriam ukiwa umezingirwa na dimbwi la damu. 

Kisu ambacho kilitumika kutekeleza mauaji yale kilipatikana kwa nyumba ile ya marehemu ambayo ilijaa ushahidi kwamba kulikuwa na vita kubwa kabla ya mshukiwa kumwangamiza marehemu.

Mshukiwa alitiwa pingu na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Lasit huku mwili wa marehemu ukipelekwa katika mochari ya Loitoktok.