Muuza duka aua jirani kwa kisu juu ya deni la shilingi 400 Bomet

Mshukiwa aliendelea na kazi yake ya kuuza duka bila wasiwasi hata baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Muhtasari

•Evans Mutai ambaye ni mmiliki wa duka moja katika eneo la Sibaiyan alitiwa mbaroni baada ya kumdunga Festus Keter kifuani kwa kutumia kisu usiku wa Jumamosi.

•Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na deni la mshukiwa la shilingi 400 ambalo ndilo lilikuwa chanzo cha mabishano makubwa kati yao.

Crime scene
Crime scene

Polisi katika kaunti ya Bomet wanamzuilia jamaa mmoja anayeripotiwa kuua jirani yake kufuatia mzozo uliohusisha deni la shilingi 400.

Evans Mutai ambaye ni mmiliki wa duka moja katika eneo la Sibaiyan alitiwa mbaroni baada ya kumdunga Festus Keter kifuani kwa kutumia kisu usiku wa Jumamosi.

Kulingana na DCI, mshukiwa aliendelea na kazi yake ya kuuza duka bila wasiwasi hata baada ya kutekeleza mauaji hayo.

Inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na deni la mshukiwa la shilingi 400 ambalo ndilo lilikuwa chanzo cha mabishano makubwa kati yao.

Mabishano yalipokuwa yamechacha Mutai alichukua kisu na kumdunga Keter kifuani na kumuacha hapo nje ya duka lake akiwa hali mahututi.Mwanakijiji mmoja ambaye aliuona mwili wa marehemu ndiye aliyepiga ripoti kwa wapelelezi katika kituo cha Chesoen ambao walifika kwenye eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Uchunguzi wa mapema ulibaini kwamba Mutai ndiye aliyekuwa ametekeleza kitendo kile na hapo ndipo akatiwa pingu na kupelekwa korokoroni.

Kisu ambacho kinadaiwa kutumika kutekeleza mauaji hayo kilipatikana na kupelekwa kituoni ili kutumika kama ushahidi mahakamani.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika mochari ya Longisa huku uchunguzi wa mwili ukisubiriwa kufanyika hivi karibuni.