Watahiniwa wawili wa KCSE taabani kwa wizi wa mitihani

Muhtasari

•Washukiwa wanaripotiwa kupatikana wamejificha kwenye choo wakiwa na simu zilizokuwa na mitihani.

•Wawili hao wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Athi River wakisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Machakos wanawazuilia wanafunzi wawili kwa madai ya kuhusika udanganyifu katika mtihani unaoendelea wa KCSE.

Wanafunzi hao wa kiume wenye umri wa miaka 19 walikamatwa siku ya Ijumaa  katika shule ya upili ya Kenanie, kaunti ndogo ya Athi River.

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Athi River mwendo wa saa kumi jioni.

Wawili hao walichukuliwa na wapelelezi wa DCI kutoka Athi River baada ya mwalimu mkuu wa shule hiyo Henry Otieno kuripoti kisa hicho.

Washukiwa wanaripotiwa kupatikana wamejificha kwenye choo wakiwa na simu zilizokuwa na mitihani.

Kulingana na polisi, maafisa wa KNEC walipata baadhi ya karatasi za mitihani zilizokuwa zimetumwa kwa watahiniwa hao kupitia mtandao wa Instagram.

Washukiwa hao wawili wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Athi River wakisubiri kufikishwa mahakamani Jumatatu.

Wapelelezi wa DCI katika kituo hicho wameanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo.