Alvin Chivondo, jamaa aliyelipiwa faini na Sonko baada ya kukiri kuiba akamatwa tena kwa wizi

Muhtasari

•Alvin Chivondo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central baada ya kukamatwa siku ya Alhamisi kwa kosa la kuiba kutoka kwa duka kubwa jijini Nairobi.

•Kinara wa ODM Raila Odinga pia ni miongoni mwa waliotoa ombi la kuachiwa huru kwa Chivondo huku akisema mshtakiwa alikuwa anajaribu kutafutia familia yake chakula.

Alvin Chivondo mahakamani
Alvin Chivondo mahakamani
Image: HISANI

Jamaa ambaye aliponea kifungo cha jela chupuchupu baada ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kulipa faini ambayo aliagizwa na mahakama kulipa baada ya kukiri kuiba katika duka ametiwa mbaroni tena kwa kosa sawia.

Alvin Chivondo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central baada ya kukamatwa siku ya Alhamisi kwa kosa la kuiba katika duka la Naivas lililo karibu na Mtaa wa Ronald Ngala,jijini Nairobi.

Chivondo ambaye sasa imebainika kuwa ni mwizi wa mara kwa mara alidaiwa kuiba unga wa mahindi katika duka hilo.

Mshukiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena baada ya polisi kukamilisha uchunguzi wao.

Wiki kadhaa zilizopita Chivondo alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja gerezani au faini ya Sh100,000 kwa kosa la kuiba kilo 5 za mchele, lita 5 za mafuta ya kupikia, kilo 2 za sukari na majani ya chai, vyote vikiwa na thamani ya Ksh3,165.

Haya ni baada yake kukiri kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani Wendy Kagendo.

Huku akijitetea Chivondo alisema alisukumwa kutenda kosa hilo kwa kuwa familia yake ilikuwa imelala njaa kwa siku tatu.

Upande wa mashtaka hata hivyo ulisema mshukiwa aliwahi kukamatawa tena kwa kosa kama hilo na kusamehewa na OCS wa kituo cha Central.

Kesi hiyo ilialika umakini wa watu wengi wakiwemo wanasiasa na wasanii mashuhuri ambao walitoa wito Chivondo aachiliwe.

Kufuatia hayo Mike Sonko alipiga hatua na kumlipa Chivondo faini yote ya shilingi laki moja.

"Pia nimeahidi kumpa hisa ya chakula cha mwezi mmoja pamoja na kumpa kazi pia." Sonko alisema.

Kinara wa ODM Raila Odinga pia ni miongoni mwa waliotoa ombi la kuachiwa huru kwa Chivondo huku akisema mshtakiwa alikuwa anajaribu kutafutia familia yake chakula.

“Alvin Linus Chivondo aachiwe huru bila masharti!. Wahalifu sasa wanapata ahueni ya kufanya kampeni kwa uhuru, huku wahalifu wadogo wakifungwa jela. Acha mahakama zipate vipaumbele vyake sawa, kwa mara moja, huwezi kumfunga mwanamume kwa kujaribu kulisha familia yake," Raila alisema.

Katika mahojiano ya hapo awali Chivondo alidai aliiba kwa kuwa mkewe na mtoto wake hawakuwa wamekula huku akisisitiza ilikuwa mara yake ya kwanza.