Kalonzo njia panda KANU ikiashiria kujiunga na Azimio

Moi alisema haya katika hafla ya kuzindua kampeni za mbunge wa Samburu Mashariki, Naisura Lesuuda

Muhtasari

• Gideon Moi wa KANU ameashiria utayarifu wao kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja na kuweka mustakabali wa OKA katika njia panda.

Kionozi wa KANU Gideon Moi na kinara wa Azimio Raila Odinga
Image: Gideon Moi (Facebook)

Kiongozi wa chama cha KANU Gideon Moi ambaye pia ni mmoja wa vinara wa muungano wa kisiasa wa OKA ameashiria kwamba huenda chama hicho kikatoa tangazo hivi karibuni la kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja unaoongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga na hivyo kuweka mustakabali wa OKA katika njia panda.

Akizungumza katika hafla ya kuzindua kampeni za mbunge wa Samburu Magharibi Naisura Lesuuda, Moi aliashiria kwamba katika mkutano wa wanachama unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni, huenda wakatangaza rasmi kuwa miongoni mwa Azimio la Umoja.

“Kwa ndugu zangu, kwa sasa unajua harakati hii ambayo sisi sote tunaelekea. Sisi kama wanachama wa KANU tuko na mrengo na nyinyi kwa hii Azimio, sisi sote tuko Pamoja. Hivi karibuni kwa maneno nyinyi wote mtasikia,” alisema Moi katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Moi pia alisisitiza kuwa iwapo wataungana na Azimio basi wawe kitu kimoja.

“Lakini tafadhali tafadhali, tukae sisi sote kitu kimoja.”

Matamshi haya ya Moi yanamweka katika njia panda kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pia analenga kuwania urais kupitia mrengo wa OKA, huku wengi wakihoji kwamba huenda hatimaye mrengo huo ukasambaratika na vinara waliosalia kujiunga na marengo mingine kama Kenya Kwanza na Azimio la Umoja.

Mrengo huo wa OKA ulianza kuyumba mapema mwaka huu pale ambapo kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa FORD-K Moses Wetengula walipogura na kujiunga na naibu rais William Ruto ambapo walianzisha muungano wa Kenya Kwanza.

Je, unahisi ndio mwisho wa reli kwa muungano wa OKA? Mustakabali wa kisiasa wa Kalonzo utakuwa upi baada ya Moi kuashiria huenda KANU  wakajiunga na Azimio?