Gavana Mwangaza kujua hatima yake wiki kesho mbele ya Maseneta

Spika Kingi alidhibitisha kuwasilishwa kwa maazimio ya bunge la kaunti ya Meru kumbandua Mwangaza.

Muhtasari

• Sheria inatoa nafasi ya siku 7 kwa seneti kujadili maazimio hayo na kutoa uamuzi iwapo Mwangaza anatimuliwa au anabaki kuwa gavana.

Gavana wa Meru akiombewa
Gavana wa Meru akiombewa
Image: Facebook

Maseneta watakutana wiki ijayo kwa kikao maalum kutafakari kuhusu kuondolewa kwa Gavana wa Meru Kawira Mwangaza.

Hii ni baada ya Spika wa Seneti Amason Kingi kupokea uamuzi wa Bunge la Kaunti ya Meru kumwondoa Gavana Mwangaza afisini. Kupokelewa kwa maazimio hayo yaliyowasilishwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru Ayub Bundi sasa kunatoa muda wa siku saba kwa kikao maalum kuitishwa kujadili suala hilo.

Spika Kingi anatarajiwa kuitisha kikao maalum cha Seneti ili kusoma mashtaka na maazimio ya Bunge la Kaunti dhidi ya gavana huyo.

Baada ya hapo, kuangazia kwa Seneti kuhusu mashtaka kutaanza, kulingana na ratiba ya nne ya Kanuni za Kudumu na Kifungu cha 33 cha Sheria ya Serikali ya Kaunti.

“Kaunti ya Meru tayari imeleta hati za kushtakiwa kwa Seneti. Tafadhali kumbuka kuwa Spika ataitisha Mkutano Maalum wa Seneti ili kusoma mashtaka na maazimio ya Bunge la Kaunti dhidi ya gavana,” yalisomeka mawasiliano kutoka Ofisi ya Spika Kingi.

Hati zilizotolewa ni pamoja na ushahidi uliotolewa wakati wa kushtakiwa pamoja na maelezo na rekodi za kesi mbele ya bunge la kaunti.

Gavana Mwangaza Jumatano jioni alitimuliwa baada ya siku 112 pekee ofisini huku MCAs wote waliohudhuria bungeni wakipiga kura kwa kauli moja kutaka serikali ya awamu ya kwanza iondolewe afisini kwa madai ya utovu wa nidhamu, utumizi mbaya wa afisi na ukiukaji mkubwa wa Katiba na sheria za kaunti.

MCAs 67 kati ya 69 walipiga kura ya ndio kushinikiza kung’atuliwa kwa gavana huyo katika kile wanakitaja kuwa ni matumizi mabaya ya ofisi na kumpa mumewe kazi katika uongozi wa kaunti.