Hang'atuki ng'o! Seneti yamwokoa Mwangaza kubanduliwa mamlakani

MCAs 67 waliandaa kampeni ya ari na kupiga kura ya kumwondoa Mwangaza ofisini.

Muhtasari
  • Kamati hiyo iliongozwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni kinara wa Wengi katika Seneti
  • Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, kamati hiyo ilielezwa jinsi gavana huyo alivyodaiwa kutumia vibaya ofisi yake kama gavana
GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: EZEKIEL AMING'A

Gavana wa Meru mnamo Ijumaa, Desemba 30 alinusurika kushtakiwa, baada ya Maseneta kutupilia mbali uamuzi wa Wabunge wa Kaunti ya Meru (MCAs) wa kumtimua.

Uamuzi huo ulitolewa katika kikao maalum kilichofanyika mchana baada ya kamati inayoongozwa na Seneta Boni Khalwale kuwasilisha ripoti kwenye sakafu ya nyumba hiyo.

Seneti ilipokea hoja iliyoidhinishwa ya kumtimua kutoka Bunge la Kaunti ya Meru dhidi ya Gavana Mwangaza mnamo Desemba 14, 2022.

MCAs 67 waliandaa kampeni ya ari na kupiga kura ya kumwondoa Mwangaza ofisini.

Wabunge hao walimshtumu kwa matumizi mabaya ya ofisi, utovu wa nidhamu uliokithiri, na ukiukaji wa Katiba.

Baada ya kupokea hoja ya kumtimua, Spika wa Bunge la Seneti Amason Kingi alibuni Kamati Maalum ya Seneti kusikiliza kesi hiyo ya kuondolewa mashtaka.

Kamati hiyo iliongozwa na Seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni kinara wa Wengi katika Seneti.

Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, kamati hiyo ilielezwa jinsi gavana huyo alivyodaiwa kutumia vibaya ofisi yake kama gavana.

Kamati iliambiwa kuwa gavana huyo alimteua mumewe kwa afisi isiyokuwapo na kukosa uwazi na ushindani katika kuajiri.

Mwangaza pia alidaiwa kudharau mchakato wa uanzishwaji wa ofisi ya mume na kushindwa kuwasilisha jina lake bungeni ili kupitishwa.

Baada ya kukamilika kwa kesi mnamo Desemba 29, Khalwale aliandika, “Tunafuraha kuhitimisha kusikilizwa kwa ushahidi katika suala la uchunguzi na kuzingatia mashtaka ya Kawira Mwangaza, Gavana wa Meru.”

"Sasa tuko katika kuandika ripoti ambayo itawasilishwa kwa seneti Ijumaa, Desemba 30," seneta huyo aliongeza.