Mwanafunzi ashtuka kwa kuuona mwili wa rafiki yake katika darasa la utafiti wa miili ya binadamu

Alipigia kelele na kutoroka kuona mwili ambao wenzake walikuwa wanakaribia kuupasua ulikuwa ule wa Devine, rafiki yake wa miaka saba

Muhtasari

•Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 26 bado anakumbuka siku ya Alhamisi jioni miaka 7 iliopita akiwa katika chuo kikuu cha Calabar nchini Nigeria , akikongamana na wanafunzi wenzake katika meza tatu ambazo zilikuwa na wafu waliokuwa wamelazwa katika kila meza.

•Bwana Egbe alituma ujumbe kwa família ya Divine ambayo ilibainika kwamba imekuwa ikimtafuta mwanao katika vituo tofauti vya polisi baada ya yeye na marafiki zake watatu kukamatwa na maafisa wa usalama walipokuwa wakitoka katika klabu za burudani.

ENYA EGBE
ENYA EGBE
Image: Hisani

Mwanafunzi anayesomea somo la matibabu Enya Egbe aliondoka katika darasa lake la utafiti wa mwili wa binadamu baada ya kusumbuliwa na mwili aliokuwa akiufanyia kazi.

Hili halikuwa tukio la kawaida kwa kijana aliyekosa uzoefu wa mambo kama hayo.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 26 bado anakumbuka siku ya Alhamisi jioni miaka 7 iliopita akiwa katika chuo kikuu cha Calabar nchini Nigeria , akikongamana na wanafunzi wenzake katika meza tatu ambazo zilikuwa na wafu waliokuwa wamelazwa katika kila meza.

Dakika chache baadaye, alipigia kelele na kutoroka. Mwili ambao wenzake walikuwa wanakaribia kuupasua ulikuwa ule wa Devine, rafiki yake wa miaka saba.

''Tulikuwa tukienda katika klabu za burudani pamoja aliniambia. ''

''Alikuwa na mashimo mawili yaliokuwa ni majeraha ya risasi katika upande wa kulia wa kifu chake''.

Oyifo Ana ni miongoni mwa wanafunzi ambao pia walitoka nje baada ya kumuona bwana Egbe akilia.

''Miili ya wafu wengi tuliokuwa tukitumia shule ilikuwa na majeraha ya risasi , nilihisi vibaya wakati nilipogundua kwamba baadhi ya watu huenda sio wahalifu'', bi Ana alisema.

Aliongezea kwamba siku moja mapema aliona gari la maafisa wa polisi likiwa limejaa miili katika shule yao , ambayo ilikuwa na chumba cha kuhifadhia maiti.

Bwana Egbe alituma ujumbe kwa família ya Divine ambayo ilibainika kwamba imekuwa ikimtafuta mwanao katika vituo tofauti vya polisi baada ya yeye na marafiki zake watatu kukamatwa na maafisa wa usalama walipokuwa wakitoka katika klabu za burudani.

Familia yake baadaye ilifanikiwa kuupata mwili wake.

kampeni ya kulivunja kundi la usalama la SARS nchini Nigeria
kampeni ya kulivunja kundi la usalama la SARS nchini Nigeria
Image: HISANI

Ugunduzi wa kushangaza wa bwana Egbe uliangazia ukosefu wa wafu nchini Nigeria ili kutumika katika masomo ya wanafunzi wanaosomea matibabu na kile kinachoweza kuwafanyikia waathiriwa wa ghasia zinazotekelezwa na polisi.

Kati ya karne ya 16 na karne ya 19, sheria tofauti nchini Uingereza ziliruhusu miili ya wahalifu waliouawa kutumika katika shule za matibabu.

Nchini Nigeria , sheria za sasa zinasema kwamba miili ambayo imekosa wenyewe katika vyumba vya kuhifadhia maiti vya serikali inapaswa kupelekwa katika vyuo vya kusomea matibabu.

Serikali pia inaweza kutumia miili ya wahalifu walionyongwa , lakini tukio la mwisho la mtu kunyongwa lilifanyika 2007.

Zaidi ya asilimia 90 ya wafu wanaotumika katika shule nchini Nigeria ni wahalifu waliouawa kwa kupigwa risasi , kulingana na utafiti wa 2011 katika jarida la matibabu kwa jina Clinical Anatomy.

Ukweli ni kwamba , hii ina maana kwamba ni washukiwa waliopigwa risasi na vyombo vya usalama. Umri wao ni kati ya miaka 20 hadi 40, ikiwa asimilia 95 ni wanaume , huku watatu kati ya wanne wakiwa watu wanaotoka katika jamii maskini.

''Hakuna lililobadilika miaka 10 baadaye'', alisema Emeka Anyanwu, profesa wa elimu ya miili ya binadamu katika chuo kikuu cha Nigeria ambaye pia ni mmoja wa waazilishi wa utafiti huo.