Vita vya Ukraine: Urusi yaishutumu Uingereza kwa kuchochea mashambulizi kwenye ardhi yake

Muhtasari

• Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema iko tayari kushambulia "vituo vya kufanya maamuzi" huko Kyiv iwapo mashambulizi kama hayo yatatokea.

Image: REUTERS

Serikali ya Urusi imeishutumu Uingereza kwa "kuichochea" Ukraine kushambulia eneo la Urusi.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema iko tayari kushambulia "vituo vya kufanya maamuzi" huko Kyiv iwapo mashambulizi kama hayo yatatokea.

Uwepo wa washauri wa nchi za Magharibi katika vituo hivyo huenda usiathiri uamuzi wake wa kulipiza kisasi, iliongeza.

Haya yanajiri baada ya waziri wa ulinzi wa Uingereza kusema "si lazima iwe tatizo" kwa Ukraine kutumia silaha zinazotolewa na Uingereza dhidi ya malengo ya kijeshi nchini Urusi.

James Heappey alisema mashambulizi ya kijeshi ya Ukraine kuvuruga njia za usambazaji bidhaa ni sehemu "halali" ya vita, na alielezea madai ya Urusi kuhusu Nato kuwa katika mzozo na Urusi kama "upuuzi".

Urusi imedai kuwa vikosi vya Ukraine vimeshambulia maeneo yaliyolengwa ndani ya ardhi yake, ikiwa ni pamoja na ghala la mafuta mjini Belgorod, lakini Ukraine haijathibitisha kuwepo kwa mashambulizi yoyote.

Nchi za Magharibi zimetoa msaada wa mamia ya mamilioni ya pauni za kijeshi kwa Ukraine tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi wake mwezi Februari, na maafisa wa Nato na Umoja wa Ulaya wamekuwa wakikutana nchini Ujerumani kujadili msaada zaidi wa kijeshi.

Serikali ya Uingereza imetangaza kuwa itavipa vikosi vya Ukraine idadi ndogo ya magari ya kuzuia ndege.

Katika taarifa iliyonukuliwa na shirika la habari la Interfax, wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema: "Tungependa kusisitiza kwamba uchochezi wa moja kwa moja wa London wa serikali ya Kyiv katika shughuli kama hizo [kushambulia eneo la Urusi], ikiwa kuna jaribio la kuzitambua, itasababisha majibu yetu sawia mara moja."

Wizara hiyo pia ilisema kuwa vikosi vya jeshi la Urusi viko tayari "kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi kwa kutumia silaha za masafa marefu zenye usahihi wa hali ya juu" dhidi ya "vituo vinavyochukua maamuzi muhimu" katika mji mkuu wa Kyiv wa Ukraine.

Waziri wa mambo ya nje Sergei Lavrov pia alishutumu Nato kwa kuendesha vita vya wakala, na kusema silaha za Magharibi zinazowasilishwa kwa Ukraine zitakuwa shabaha za haki.

Bw Lavrov alidai kuwa nchi za Magharibi "zinamwaga mafuta kwenye moto" kwa kuipatia Ukraine nguvu ya kuzima moto, na kuonya mara kwa mara kwamba mzozo huo unaweza kusababisha vita vya tatu vya dunia.