Mganga wa kiasili ahukumiwa kunyongwa kwa kulawiti na kuua watoto 2

Mganga huyo alipatikana na hatia ya kuwafanyia ukatili watoto hao wa miaka 7 na 4 kabla ya kuwaua.

Muhtasari

• Mganga huyo mwenye umri wa miaka 57 alipatikana na hatia baada ya kesi yake kuendeshwa kwa zaidi ya miaka 3 tangu tukio hilo kutokea Machi 2019.

Kamba ya kujiua
Kamba ya kujiua
Image: Image: Courtesy

Je, unaamini kuna mahakama katika bara la Afrika zinzotoa hukumu za kifo kwa kunyongwa watuhumiwa, na kama zipo, kuna ukweli gani kuwa uamuzi huo hutekelezwa?

Nchini Tanzania, mahakama moja katika kanda ya Sumbawanga imegonga vichwa vya habari Afrika Mashariki baada ya hakimu kumhukumu mganga mmoja wa jadi kunyongwa.

Mganga huyo aliyetambulika kwa jina James Kapyela mwenye umri wa miaka 57 alipatikana na hatia ya kuwaua watoto wawili wa kiume wenye umri wa miaka 7 na 4 mtawalia katika kile mahakama ilisema ni kwa makusudi kabisa.

Mahakama ilibaini kwamba mganga huyo aliwafanyia ukatili watoto hao kwa kuwalawiti kabla ya kuwaua na kutupa miili yao kwenye eneo moja nyumbani kwake miaka 3 iliyopita.

Kulingana na jarida la Mwananchi nchini humo,  Jaji Thadeo Mwenempazi alisema wakati akisoma hukumu hiyo Jumanne Oktoba 26, 2022 kuwa mahakama iliridhika kuwa mashahidi 11 wa Jamhuri wamethibitisha mashtaka dhidi ya mganga huyo.

Kabla ya kuthibitika kuuawa, watoto hao walitoweka nyumbani kwao na kuwafanya wazazi na majirani kuanzisha juhudi za pamoja kuwatafuta huku wakitoa taarifa katika Kituo cha Polisi, Sumbawanga Mjini.

Ilidaiwa kuwa siku iliyofuata binti mmoja aliyekuwa amekwenda mtoni kuteka maji alidai kumwona mmoja wa watoto walipotea na kutoa taarifa kwa wazazi wa watoto hao.

Uchunguzi wa kitabibu ulionesha kuwa watoto hao walilawitiwa kabla ya kunyongwa.

Jaji Mwenempazi alisema kuwa alilazimika kutoa hukumu ya aina hiyo kufuatia  kifungu cha 196 had 197 cha Kanuni ya Adhabu katika katiba ya Tanzania kinachotoa adhabu moja tu ya kunyongwa hadi kufa kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kuua kwa makusudi.