Mwanamke amtoa kafara mtoto wake wa miezi 2 kwa kumzika akiwa hai

Mama huyo alishrutishwa na mganga ambaye ni shemeji yake kufanya kitendo hicho cha uhaini.

Muhtasari

• Shemeji yake ambaye ni mganga alimwambia kuwa angemzika mtoto wake basi wangepata neema ya utajiri.

Mtu alifukiwa akiwa hai
Mtu alifukiwa akiwa hai
Image: The Live Nugpur, Getty Images

Mwanamke mmoja amegonga vichwa vya habari baada ya kudaiwa kumzika mtoto wake mchanga akiwa hai, kwa lengo la kumtoa kafara ili apate utajiri.

Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina Zawadi Michael Msagaja mwenye umri wa miaka 20 kutoka mkoa wa Mwanza nchini Tanzania alikamatwa pamoja na mganga wa kienyeji pamoja na babake.

Kamanda wa polisi Wilbroad Mutafungwa katika video ambayo ilipakiwa mitandaoni alidhibitisha kisa hicho na kusema watuhumiwa wapo chini ya vyombo vya dola huku uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo lisilo la kawaida ukiendelea.

“Zawadi Msagaja alikuwa akiishi na dada yake, aliamriwa na shemeji yake, ambaye ni mume wa dadake, ambaye ni mganga wa kienyeji. Alimuamuru amtoe kafara mtoto wake wa jinsi ya kike mwenye umri wa miezi miwili,” kamanda huyo alsiema.

Shemeji huyo mganga alimpa hakikisho kuwa pindi angemaliza kufanya hivyo basi wote watatu kwa maana ya mama mtoto, dadake na mume wa dadake wangevuna utajiri wa kiasi kikubwa kutokana na kumzika mtoto akiwa hai.

Jeshi la polisi liliendelea kueleza kuwa mganga huyo alimpa mama mtoto vitisho na kumshrutisha kufanya hivyo kwani angekosa kutekeleza uamuzi wa mganga basi yeye mwenyewe angeingia kwenye matatizo makubwa, hadi kupoteza maisha.

Baada ya tukio hilo, mganga aliweza kutoroka.

Polisi baada ya kufukua kaburi, walimpata mtoto huyo lakini kwa bahati mbaya alikuwa amepoteza maisha.