Mahakama ya upeo yabatilisha uchaguzi wa Mbunge wa Magarini na kuamuru uchaguzi mdogo

Kombe aliagizwa kulipa mlalamishi Stanley Kenya gharama ya kesi isiyozidi shilingi milioni mbili.

Muhtasari

• Majaji waliamuru kwamba IEBC itangaze kiti cha Mbunge wa Magarini wazi mara moja na kuandaa uchaguzi mdogo kwa mujibu wa sheria.

Mbunge wa Magarini Harrison Kombe Picha: MAKTABA
Mbunge wa Magarini Harrison Kombe Picha: MAKTABA

Mahakama ya upeo imebatilisha uchaguzi wa Agosti 9, 2022 wa Mbunge wa Magarini Harrison Kombe.

Majaji Smokin Wanjala, Njoki Ndungu na Mohammed Ibrahim siku ya Ijumaa walibaini kuwa Kombe, ambaye aligombea kwa tikiti ya ODM, alijihusisha na kujaza kura na kubadilisha matokeo ya uchaguzi.

Jopo hilo lilikubaliana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba kulikuwa na ukiukaji wa katiba hatua ambayo iliathiri matokeo ya mwisho, kwa kuzingatia vipengele vyote viwili vya Kifungu cha 83 cha Uchaguzi.

“Kwa sababu hiyo, hatuoni msingi wa kukata rufaa, kwa hivyo inatupiliwa mbali na ili kuepusha mashaka, tunathibitisha uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, pamoja na maelekezo. Wadhifa wa mbunge wa Magarini uko wazi na kuagiza kufanyika kwa uchaguzi mdogo kwa mujibu wa sheria," majaji waliamua.

Majaji waliamuru kwamba IEBC itangaze kiti cha Mbunge wa Magarini wazi mara moja na kuandaa uchaguzi mdogo kwa mujibu wa sheria.

Kombe aliagizwa kulipa mlalamishi Stanley Kenya gharama ya kesi isiyozidi shilingi milioni mbili.

Kombe alimshinda Stanley Kenga wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa kura 21 pekee. Alipata kura 11,946 dhidi ya 11,925 za Kenga.

Michael Kingi wa Chama cha Pamoja African Alliance (PAA) aliibuka wa tatu kwa kupata kura 7,921.

Kenga wa UDA aliwasilisha ombi katika Mahakama Kuu akitaka kubatilishwa kwa ushindi wa Kombe kwa madai ya ubadhirifu wa uchaguzi.

Kombe alihudumu kama mbunge kwa mihula miwili kuanzia 2007-2013 na 2013-2017.