Wafahamu waigizaji wa awali wa Tahidi High ambao wameendelea kubobea kwenye sanaa

Drama ambazo zimemzingira Omosh zimeibua maswali kuhusu hatima ya waliokuwa waigizaji wenzake kwenye kipindi cha Tahidi High.

Muhtasari

•Kipindi hicho kilishirikisha waigizaji mashuhuri ambao walipata umaarufu mkubwa na kusherehekewa sana na Wakenya.

•Baada ya kuondoka Tahidi High, Makena  aliamua kufuata shauku yake ya kucheza santuri. Kwa sasa yeye ni mcheza santuri mashuhuri sana akijulikana kwa jina la usanii kama DJ Pierra Makena.

Waigizaji wa Tahidi High
Waigizaji wa Tahidi High
Image: Hisani

Tahidi High ni kipindi ambacho kilitumbuiza Wakenya kwa miaka mingi. Kipindi hicho kilionyeshwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2006.

Kipindi hicho kilishirikisha waigizaji mashuhuri ambao walipata umaarufu mkubwa na kusherehekewa sana na Wakenya.

Hata hivyo, walikoenda waigizaji hao baada ya kuondoka Tahidi High ni swali ambalo Wakenya wengi wamejiuliza haswa baada ya masaibu yaliyomkumba mmoja wao kwa jina Joseph Kinuthia almaarufu kama Omosh.

Drama ambazo zimemzingira Omosh zimeibua maswali kuhusu hatima ya waliokuwa waigizaji wenzake kwenye kipindi cha Tahidi High.

Hivi majuzi, Omosh amekuwa akiwaomba msaada wa Kenya huku akisema kuwa ana shida nyingi ambazo amekuwa akipambana nazo.

Marafiki na watu walio karibu naye wamefichua kuwa mwigizaji huyo alijitosa kwenye uraibu wa pombe na juhudi za kurekebisha mienendo yake hazijafua dafu.

Hata hivyo, kuna baadhi ya waigizaji wa kipindi cha tahidi high ambao wameendelea kubobea kwenye ulingo wa sanaa. 

Hawa hapa wasanii ambao nyota yao imeendelea kung'aa hata baada ya kuondoka Tahidi High;

 

1. Abel Mutua

Mutua ni baadhi na waigizaji mashuhuri na waliobobea  sana nchini hadi wa sasa.

Alicheza kwenye kipindi cha Tahidi High kama Freddy kuanzia mwaka wa 2007.

Kwa sasa  Mutua ni mmiliki mwenza wa kampuni ya kutengeneza filamu ya Phil-it ambayo wanamiliki pamoja na Philip Karanja.

Baada ya kuondoka Tahidi High, Mutua aliendeleza taaluma yake ya uigizaji na amekuwa mhusika kwenye filamu na vipindi mbali mbali kama Sue na Johnie, Crime and Justice, Anda Kava na nyinginezo.

Mbali na hayo, Mutua ni mwandishi wa filamu na ameandika filamu kadhaa zilizovuma kama vile Real Househelps of Kawangware, Sue na Joni na Anda Kava.

Sarah Hassan na Abel Mutua
Sarah Hassan na Abel Mutua
Image: Instagram

2. Sarah Hassan

Sarah Hassan ni mmoja wa wasanii ambao walipata umaarufu mkubwa kutokana na kipindi cha Tahidi High.

Mwigizaji huyo wa miaka 32 alicheza kama 'Tanya' kwenye kipindi hicho takriban miaka 10 iliyopita.

Alikuwa mmoja wa waigizaji bora kwenye kipindi cha Tahidi High huku akipokea tuzo la Chaguo la Teeniez mwaka wa 2011 kwenye kitengo cha mwigizaji bora wa kike.

Baada ya kuondoka Tahidi High mwaka wa 2011, Sarah aliendelea na taaluma yake ya uigizaji na ameshirikishwa kwenye filamu mbalimbali kama vile House of Lungula(2013), Jane & Abel(2014), Plan B(2019).

Mwaka huu amecheza kama Muthoni kwenye filamu ya Just in Time na anacheza kama Zora kwenye kipindi cha Zora kinachoonyeshwa kwenye runinga ya Citizen.

Hassan pia ni mtangazaji wa runinga.  Alitangaza kipindi cha densi cha Sakata , mwaka wa 2013-2014 akatangaza kipindi cha Wedding Show katika Citizen TV , Discovery +254 ya NTV na hivi karibuni Mashariki Mix ya Maisha Magic TV.

3. Philip Karanja

Karanja alijulikana kama Melvin kwenye kipindi cha Tahidi High.

Kwa sasa msani huyo anamiliki kampuni ya kutengeneza filamu ya Phil-it na pia ni mwelekezi wa filamu pale.

Karanja ameelekeza filamu na vipindi mbalimbali zilizovuma sana nchini kama Sue na Johnie, The Real Househelps of Kawangware na Aphrodite.

Licha ya kuhitosa sana kwenye taaluma ya kuelekeza filamu, Karanja bado hajatupilia mbali uigizaji wake.

4. Pierra Makena

Pierra Makena
Pierra Makena
Image: Instagram

Makena anajulikana sana kutokana na kucheza santuri kwake. 

Kwenye kipindi cha Tahidi High, Makena alijulikana kama Jean Joyce. Kando na Tahidi High, Makena alicheza kwenye kipindi cha Tausi kilichokuwa kinaonyeshwa KBC.

Baada ya kuondoka pale aliamua kufuata shauku yake ya kucheza santuri. Kwa sasa yeye ni mcheza santuri mashuhuri sana akijulikana kwa jina la usanii kama DJ Pierra Makena.

Hata hivyo, Makena hakutupilia mbali uigizaji wake kwani amecheza kwenye filamu mbalimbali kama When Love Comes Around (2014) na Disconnect(2018).

5. Shirleen Wangari

Wangari alijulikana kama Shish kwenye kipindi cha Tahidi High. Kipindi  hicho kilimfungulia njia mwigizaji huyo tajika.

Baada  ya kuondoka Tahidi High, Wangari aliendeleza uigizaji wake. Amehusika kwenye filamu nyingi za kimataifa zikiwemo Peponi, A perfect plan, Subira, The First grager, Sense 8, 18 hours kati ya zingine.

Kwa sasa Wangari ni mtengenezaji filamu katika kampuni ya Blackwell Films Limited.