Wafahamu wanaharakati wanaozikosesha usingizi Serikali za Afrika Mashariki

Mara nyingi mwanaharakati au wanaharakati hutazamwa kama wakosoaji wakubwa wa serikali ama mamlaka za nchi.

Muhtasari

•Uanaharakati ni neno la kiarabu lenye maana ya mchakato wa mtu ama watu kufuatilia jambo fulani wanaloamini lina maana ama la msingi kwa maisha ya jamii.

•Mwezi Februari mwaka huu  Stella Nyanzi  alikimbilia Kenya kunusuru maisha yake, baada ya kuvamiwa na kuteswa na watu wanaoonekana kutokubaliana na matendo yake, wengi wanawaona kama wanatumwa na mamlaka kumzima mdomo.

•Huenda ikawa Okiya Omtatah ndiye mwanaharakati aliyefungua kesi nyingi zaidi nchini Kenya dhidi ya masuala yanayokwenda kinyume na katiba, na si aghalabu siku moja kumkuta kwenye rekodi za kitabu cha Guinness kwa mtu aliyefungua kesi nyingi zaidi.

Image: HISANI

Uanaharakati ni neno la kiarabu lenye maana ya mchakato wa mtu ama watu kufuatilia jambo fulani wanaloamini lina maana ama la msingi kwa maisha ya jamii.

Askofu mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Benson Bagonza anatafsiri uanaharakati kama imani na ushawishi (conviction and commitment) katika jambo fulani analosimamia mtu na kulipigania.

Mara nyingi mwanaharakati au wanaharakati hutazamwa kama wakosoaji wakubwa wa serikali ama mamlaka za nchi.

Na kwa nchi nyingi hasa za Kiafrika watu hawa huonekana kama maadui wa mamlaka na wakati mwingine hupitia maisha na wakati mgumu wa kutekeleza majukumu yao na kufikia malengo yao.

Wengi wao ni wanaharakati wanaotetea haki za binadamu kwa misingi ya kuhakikisha hasa mamlaka hazivunji haki hizo.

Wako wanaharakati wengi Afrika mashariki wanaoonekana mwiba kwa mamlaka , miongoni mwao ni hawa:

Fatma Karume kutoka Tanzania

Image: FATMA KARUME

Huyu ni mwanaharakati kutoka katika familia ya viongozi; babu yake Shekhe Abeid Karume alikuwa muasisi na Rais wa kwanza wa Zanzibar, baba yake Aman Abeid Karume alikuwa rais wa awamu ya saba wa visiwa hivyo huku baba yake mdogo Ally Abeid Karume amewahi kuwa balozi na waziri katika awamu za serikali mbalimbali.

Fatma maarufu kama Shangazi kitaaluma ni mwanasheria aliyezaliwa Juni 15, 1969, na amekuwa mwanaharakati wa muda mrefu akitumia taaluma yake ya sheria katika kufanya shughuli zake za uanaharakati.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alianza kusoma sheria huko Strasbourg, Ufaransa hadi 1991. Mwaka 1992 akaendelea kupata shahada ya awali ya sheria kwenye Chuo Kikuu cha Sussex.

Kukuliwa kwenye familia ya viongozi au kuwa mtoto wa rais mstaafu na mjukuu wa muasisi wa taifa hilo, pengine kungemfanya kuunga mkono masuala mengi yanayofanywa na serikali inayoongozwa na chama cha mapinduzi (CCM), ambacho wazazi wake wamekuwa wanachama kwa muda mrefu, lakini imekuwa tofauti.

Amekuwa mkosoaji mkubwa wa hatua nyingi zilizofanywa na zinazofanywa na utawala wa chama hicho, na kujikuta kwenye dhahma za mara kwa mara na mamlaka.

Ofisi yake ilipigwa bomu ikiwa ni moja ya mashambulio dhidi yake. Alifukuzwa katika Kampuni ya Uanasheria ya IMMMA Advocates aliyoshiriki kuianzisha.

Akieleza kufukuzwa kwake, anahusisha na harakati zake.

"Hii ni kuwajulisha nyote kwamba, nimefukuzwa kwenye ofisi niliyoijenga. Uovu wangu, uanaharakati," aliandika Fatma kwenye ukurasa wake wa twitter Septemba 21 mwaka 2020.

Aliondolewa pia uraisi wa chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) kabla ya kufutwa kabisa kwenye orodha ya mawakili ili asiweze kufanya kazi za uwakili nchini humo hasa bara kulikotolewa hukumu hiyo. Lakini hii haijamzuia Fatma kuendelea na msimamo wake na harakati zake.

Maria Sarungi kutoka Tanzania

Image: MARIA SIRUNGI

Ni mwanaharakati aliyejikita zaidi kwenye kutaka mabadiliko akitumia mitandao ya kijamii zaidi kutekeleza azma yake hiyo.

Kampeni iliyompa umaarufu zaidi ni "Change Tanzania" iliyoanza kama hashTag kwenye mtandao wa Twitter, na kwa sasa amekuwa akiendesha mijadala mikubwa inayohusisha maelfu ya Watanzania kupitia jukwaa la "Space" la Twitter.

Mijadala hii kwa kiasi kikubwa inakosoa mamlaka kwenye maeneo mbalimbali, lakini pia inachochea ushawishi wa masuala mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya katiba ya nchi, kuondolewa kwa sheria kandamizi na kuchochea uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.

Maria amekuwa akiendesha shindano la urembo la Miss Universe Tanzania akiwa ni mtaalam wa mawasiliano na uandishi wa habari, na mmiliki wa kampuni ya Compass communication.

Amekua akisimamia midahalo mbalimbali ikiwemo ya uchaguzi kupitia kampuni yake.

Kupitia juhudi na uanaharakati wake aliteuliwa na aliyekuwa rais wa Tanzania wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa bunge la katiba mwaka 2014.

Kituo chake cha Kwanza TV kimekumbana na rungu la kufungiwa kutokana na maudhui yake yaliyoonekana kwenda kinyume cha sheria, Mijadala anayoiendesha na jumbe zake hasa kwenye mtandao wa twitter zimekuwa homa kali kwa mamlaka.

Stella Nyanzi kutoka Uganda

Image: HISANI

Ni msomi wa elimu ya juu na Profesa asiyeogopa kusema lolote analoamini tena wakati wowote hata kama linamuhusu Rais wa nchi.

Amekaa jela mara kadhaa kwa harakati zake dhidi ya mamlaka za Uganda. Alikuwa na kesi ya kumtukana Rais Museveni.

Alikaa jela kwa miezi 18 lakini kama haikutosha alipotoka tu akasema

"Museven lazima uondoke, nakupa notisi, uondoke, unaweza kufanya lolote tuko tayari, tumechoka, Museven, acha kukandamiza Waganda".

Aliwahi pia kukaa ndani kwa siku 33 kwa kuchapisha kwenye mtandao wake wa Facebook ujumbe unaodaiwa kumtusi Rais Museveni.

Akiwa jela aliandika ushairi matata ambao ulisambaa na kukimbiliwa na wengi kutokana na maudhui yake ya kiuanaharakati.

Mwezi Februari mwaka huu alikimbilia Kenya kunusuru maisha yake, baada ya kuvamiwa na kuteswa na watu wanaoonekana kutokubaliana na matendo yake, wengi wanawaona kama wanatumwa na mamlaka kumzima mdomo.

Okiya Omtata kutoka Kenya

Okiya Omtata
Okiya Omtata
Image: HISANI

Huyu ni mwanaharakati kutoka nchini Kenya aliye mstari wa mbele kupinga maamuzi yoyote yanayokwenda kinyume na katiba ya nchi.

Huenda ikawa ndiye mwanaharakati aliyefungua kesi nyingi zaidi nchini Kenya dhidi ya masuala yanayokwenda kinyume na katiba, na si aghalabu siku moja kumkuta kwenye rekodi za kitabu cha Guinness kwa mtu aliyefungua kesi nying zaidi.

Okiya alizaliwa katika kaunti ya Busia November 30, 1964, na kujiunga na sekondari ya st Paul na huko akakutana na mchungaji ambaye ndiye aliyemshawishi kuwa alivyo leo.

Kabla ya kujiunga na shule ya Sekondari mtakatifu Peters School huko Mukumu alipomaliza elimu ya juu ya sekondari mwaka 1983.

"Uanaharakati nilianza nikiwa Sekondari ingawa nilikuwa mtiifu na mwenye heshima lakini nilikuwa nahoji sana, na ni wakati huo nilipoanza kuona umuhimu wa uhuru wa kujieleza".

Boniface Mwangi kutoka Kenya

Boniface Mwangi akikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuongoza maandamano
Boniface Mwangi akikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuongoza maandamano
Image: GETTY IMAGES

Boniface Mwangi akikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuongoza maandamano

Huyu ni mwandishi wa habari akibobea zaidi katika taaluma ya upigaji picha. Nadharia ya picha inamleta katika maisha halisi ya kupigania haki mbalimbali za watu.

Ameshinda tuzo mbalimbali za kimataifa kwa kazi zake za kuonyesha udhaifu na ukiukwaji wa haki za binadamu lakini amekuwa akiamini kuwa ili kulinda uhuru wa kujieleza nchini Kenya ni lazima watu wengi zaidi watashiriki.

"Kama kila mtu atashiriki hakika nani atakayemuua mwingine?"

Kwa sababu ya uanaharakati wake na kesi zake nyingi dhidi ya mamlaka, Mwangi amekuwa akizinyima usingizi mamlaka za nchini kenya.