Jinsi Rais Kenyatta alivyomshambulia DP Ruto katika mkutano wa Sagana III

Muhtasari

•Rais Kenyatta alitumia fursa hiyo kumpendekeza kinara wa ODM Raila Odinga kuwa rais wa tano wa Jamhuri wa Kenya na kuwageuza wakazi wa eneo analotokea dhidi ya naibu wake William Ruto.

•Rais  alisikika akimshambulia naibu wake kwa miaka tisa, William Ruto kuhusu masuala mbalimbali hasa yanayohusu ufisadi.

Jinsi Rais Kenyatta alimshambulia DP Ruto
Jinsi Rais Kenyatta alimshambulia DP Ruto
Image: MAKTABA

Siku yaJumatano Februari 23, Rais Kenyatta aliwakaribisha viongozi wa eneo la Mlima Kenya katika  Sagana State Lounge kwa mara ya tatu tangu utawala wake kung'oa nanga.

Rais alitumia fursa hiyo kumpendekeza kinara wa ODM Raila Odinga kuwa rais wa tano wa Jamhuri wa Kenya na kuwageuza wakazi wa eneo analotokea dhidi ya naibu wake William Ruto.

Alisema kuwa kinara wa ODM Raila Odinga ndiye chaguo bora la rais katika uchaguzi wa mwaka huu huku akidai kuwa Ruto anafaa kubadili mienendo yake kabla ya kupatiwa kiti hicho kikubwa zaidi nchini.

"Nawaomba tumshike mkono mzee huyo (Raila Odinga)  tumsukume apite tuendelee mbele. Hata kijana huyo wangu (Ruto) wakati atakuwa sawa  huko mbele arudi, mimi sina shida. Sijanyima mtu yeyote lakini hapa tuende inavyofaa" Rais alisema.

Kabla ya kumpendekeza Raila, Rais Kenyatta alisikika akimshambulia naibu wake kwa miaka tisa, William Ruto kuhusu masuala mbalimbali hasa yanayohusu ufisadi.

Rais alimstumu naibu wake na wandani wake kwa kwa kuwarubuni viongozi wa kanisa kwa kutumia pesa za wizi ili wampigie debe.

"Unakuja hapa na pesa ambazo zilifaa kujengea watu wa Elgeyo Marakwet  bwawa, bilioni tatu, ili watoto wa Mungu waweze kunywa maji, ili watoto wa Mungu waweze kulima. Pesa hizo  ziliwekwa kwa mfuko ya mtu alafu anakuja kusimama mbele ya kanisa na kusema nimemkabidhi milioni mbili. Unakuja hapa kutuimbia Halelluyah! Chukueni pesa za kweli" Rais alisema.

Rais pia alimkashifu naibu wake kwa kuendelea kukosoa utawala wale huku akidai kwamba yeye pamoja na wandani wake walishindwa kufanya kazi walipokuwa na nafasi.

Alisema kuwa Mudavadi, ambaye ni mmoja wa wanaomuunga Ruto mkono alishindwa kuboresha uchumi alipokuwa waziri wa fedha. Vilevile alisema sekta ya kilimo ilikuwa inafanya vibaya wakati ilikuwa mikononi mwa Ruto na washirika wake.

 "Nani amekuwa akiongoza wizara ya kilimo? Ni mimi ama ni wao?? Mwaka mmoja unusu wa utawala wa  Munya maendeleo yameonekana.  Alafu mnatuambia eti mtakuja kutengeneza, mnakuja kutengeneza mahali ambako mlishindwa kutengeneza miaka hiyo  yote mliishi huko?!" Rais alisema.

Rais Kenyatta pia alimkosoa Ruto  kwa kuangazia kampeni zake zaidi na kusahau kazi yake kama naibu rais wa nchi wa Kenya. Kenyatta alisema kuwa naibu rais na wanadani wake wamekuwa wakizunguka nchi wakifanya kampeni na na hawajatenga muda wa kufanya kazi. 

"Huwa wanapatia vijana hadithi wakiwa juu ya gari. Wale ambao wanaimba juu ya gari huwa hawaingii kwa ofisi yoyote, hakuna kazi ambayo huwa wanafanya. Kazi yao ni kutusiana tu. Sina chuki na mtu lakini heri mzee aliyekaa chini kuliko kihii (kijana mdogo ambaye hajatahiriwa) aliye juu ya mti. Acha mimi nikae na mzee wangu (Raila)," Rais alisema.

Vilevile rais alimkashifu naibu wake pamoja na wandani wake kwa kuendea kukosoa uamuzi wake kufanya kazi na Raila Odinga na kujitenga na serikali.