Simulizi: Nilimkaribisha dadangu mdogo kwangu, akaja na kunipokonya mume wangu - video

"Mwanzoni nilikuwa nafikiria ni mapenzi ya mtu na shemeji yake, nikitoka chumba cha kulala nawapata sebuleni amemwekelea mkono na akiniona anatoa…"

Muhtasari

• Mrembo huyo licha ya kukaa kwenye ndoa kwa miaka 5, alisema mumewe hajawahi mpeleka kwao, na wana watoto wawili.

• Alisema kuwa pia anashuku mumewe na yeye ni ndugu wa damu kwani shangazi ya mumewe alipowatembelea walifahamiana naye akashangaa, majina ya baba zao yote yanafanana.

Mrembo huyo upande wa kushoto alisimulia kwamba dadange [kulia] alikuja kuishi nao kwake lakini mwisho wa siku akamchukulia mke.
Mrembo huyo upande wa kushoto alisimulia kwamba dadange [kulia] alikuja kuishi nao kwake lakini mwisho wa siku akamchukulia mke.
Image: Screengrab

Mrembo mmoja katika msururu wa video kwenye mtandao wa TikTok ameelezea jinamizi ambalo limekuwa likiandama ndoa yake, baada ya kumkaribisha dadake mdogo kuishi naye.

Mrembo huyo alikuwa akimuelezea jamaa mmoja ambaye alimuita kama mpatanishi wa Amani katika nyumba yake, hii ni baada ya kushuku kwa muda mrefu kwamba dadake mdogo ambaye alimkaribisha kuishi nao, anatoka kimapenzi na bwanake.

Kwa mujibu wake, anaeleza kwamba akili zake zimetatizika baada ya kugundua hilo, na kuongeza msumari moto kwenye kidonda, bado anashuku kuwa yeye na bwanake huenda ni watu wa ukoo mmoja. Kivipi?

Kwa suala la kushuku uhusiano wa kiukoo, mwanamke huyo mama wa watoto wawili alieleza kwamba kuna kipindi shangazi ya bwanake aliwatembelea na walipopata nafasi ya kuwa na maongezi ya kike naye, walifahamiana kwa undani, kipindi hiki bwanake alishatoka.

Shangazi wa bwanake alishangaa sana mama huyo alipomuelezea kuhusu kwao, majina ya ukoo na hadi kugundua kwamba jina la babake na la bwanake ni sawa.

Shangazi mtu alimtaka mrembo huyo kuchunguza sana, huku akimsisitiza kwamab huenda kuna uwezekano mkubwa kuwa yeye na mume wake wametoka kwa baba mmoja.

“Kuna hiyo siku auntie yako amekuja hapa tukaongea na yeye. Na vile alitoka alikuwa na habari zote kuhusu mimi na wazazi wangu. Na nikamuelezea vizuri kwenye wametoka, kwenye nimezaliwa, mama yangu na babangu wanaitwaje. Na akaniambia nichunguze sana kuhusu majina yetu ya baba juu yanafanana. Akasema kuna uwezekano yeye ni kakangu,” mrembo huyo alisema baina ya machozi.

Lakini alipojaribu kumketisha mumewe chini ili kulijadili, mumewe alionekana mkaidi kupita kiasi akisema kuwa amemzoea mkewe na nginjera zake, na kuwalaumu marafiki zake kwa kile alisema ni kumharibu mkewe.

“Unasikia vitu anasema, huyu mwanamke nimemzoea. Wewe mambo yangu ni ngumu. Sijui kama ni marafiki zake wamemharibu,” alisema jamaa huyo.

Katika jambo la pili na ambalo limemsumbua Zaidi mwanamke huyo, alisema kuwa alimkaribisha dadake kuishi naye lakini dadake huyo alifika na kuanza kutoka kimapenzi na bwanake, na hadi kusimulia jinsi alijiaminisha baada ya kuwashuku kwa muda mrefu.

“Mimi nimekuwa nikishuku kuhusu bwanangu na dadangu, lakini mwanzoni nilikuwa nafikiria ni mapenzi ya mtu na shemeji yake, nikitoka chumba cha kulala nawapata sebuleni amemwekelea mkono na akiniona anatoa… huyu dadangu nilimuita tu sababu nyumbani shule alikuwa anaenda tulimbadilisha,” alisema.

Bwanake alipofika mwafaka haukufikiwa baada ya kuwaitisha wote simu – mumewe na dadake – na wote wakadinda kutoa simu zao.

Lakini mama huyu alisisitiza kwamba wanamzunguruka kimapenzi, na mumewe akikana vikali na kusema kuwa hakuna kilichokuwa kinaendelea kati yake na shemeji yake.

Na dadake mwanamke huyu pia naye alisema kuwa hakuna kinachoendelea kati yake na mume wa dadake, lakini akakataa kutoa simu, jambo lililosababisha kivangaito kikali katika nyumba hiyo, mpatanishi akilazimika kuingilia kati kutuliza hali.

Licha ya kuoana kwa miaka 5, mwanamke huyo alisema kuwa mumewe hajawahi mpeleka nyumbani kwao na taarifa za shangazi ya bwanake zilimtia wasiwasi mkubwa kuwa huenda ni wakawa ndugu.

Alisema amejaribu kumzungumzia mumewe kuhusu hilo lakini amekuwa mtu wa kumpuuzilia mbali akisema amemzoea.

Huu hapa ni mfululizo wa simulizi hiyo ya kustaajabisha kweli;